Na, Ruth Kyelula, Manyara RS
Naibu Waziri, Wizara ya Maji, Eng. Mathew Kundo (MB) amesisitiza juu ya ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira Mkoani Manyara, hasa Wilayani Hanang' ambapo miradi mingi ya maji inatekelezwa.

Aliyasema hayo Februari 11, 2026, wakati akizindua Mpango wenye gharama za uwekezaji wa huduma za maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi (WASH), ambapo umezinduliwa Wilayani Hanang', Mkoani Manyara.

Aidha amesema kuwa, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na sekta binafsi, imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

"Huu ni utekelezaji kwa vitendo wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia maboresho yaliyofanyika katika sera ya Taifa ya maji na ya mwaka 2002 Toleo jipya la mwaka 2025 ambapo imesisitiza mashirikiano ya Serikali na sekta binafsi katika kuboresha huduma za maji safi na usafi wa mazingira." Alisema Eng. Kundo.

Naibu Waziri, aliendelea kusema kuwa, Mpango wenye gharama za uwekezaji wa maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi (WASH) wa miaka miaka mitano (2026 - 2030) unaolenga kupanua huduma za maji, kuboresha miundombinu ya usafi wa mazingira na kuimarisha usimamizi wa WASH katika jamii Wilayani Hanang' unalenga kuongeza upatikanaji wa maji safi hadi angalau asilimia 95 na kuhakikisha shule zote na vituo vya kutolea huduma za afya vinakuwa na huduma za msingi za WASH, hatua ambayo itakayochangia kuboresha afya na ustawi wa wananchi.

Kwa upande wake Mbunge wa Hanang', Asia Halamga, amewashukuru Water Aid Tanzania, kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Wilaya yao, na pia amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumfikishia kila mwananchi maji ndani ya nyumba yake.

Nae Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Almishi Hazali, aliwapongeza Water Aid Tanzania kwa kuleta miradi ya maji Hanang' na kusema kuwa Wilaya ina Kata 33 na mpaka sasa ni vijiji 20 tu ndio vilivyokosa maji na amemuomba Naibu Waziri awasaidie kuongea na TANESCO pamoja na RUWASA waungane ili kuweza kumtua mama ndoo kichwani kwa asilimia mia moja.

Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.