Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, imefanya ukaguzi na kuridhishwa na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, inayojengwa katika kata ya Dongobesh wilayani Mbulu.
Akieleza kuridhishwa kwake na hatua ya ujenzi na matumizi sahihi ya fedha za Serikali, Mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt, Jason Rweikiza amesema Kamati ya Bunge imeridhishwa na hatua ya ujenzi kwa kuzingatia ubora na thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali, na kuitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI, kuhakikisha fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya Hospitali hiyo zinatolewa haraka ili kukamilisha miundombinu iliyobaki ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma iliyokusudiwa.
Wakati huo huo Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mwita Waitara ameihakikishia Kamati hiyo kuwa, Wizara ya TAMISEMI inafuatilia kwa makini ujenzi wa Hospitali zote 67 za Wilaya zinajengwa kwa awamu ya kwanza kwa ukaribu na kuhakikisha zinaanza kufanya kazi, pamoja na kuhakikisha ushauri wote uliotolewa na Kamati unazingatiwa na kufanyiwa kazi.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Dkt Chitopela amesema, Hospitali hii ni tegemeo kubwa kwa wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kwa kuwa inategemea kuhudumia wakazi zaidi ya 220,000, na kupunguza adha kubwa ya wananchi wanao safiri umbali mrefu kufuata huduma ya afya. Kwa upande wa wananchi wa Mbulu wamemshukuru sana Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kuwakumbuka na kuwaondolea adha kubwa katika sekta ya afya na hakika wamepata mkombozi na kiongozi anayejali maisha yao.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.