Mkoa una jumla ya vituo 230 vya kutolea Huduma za Afya hadi kufikia mwezi Septemba, 2021. Kati ya hivyo kuna Hospitali 12 zikiwemo 8 za Serikali na 4 za Mashirika ya Dini. Vituo vya Afya vipo 29 kati ya hivyo 22 ni vya Serikali na 7 ni vya Binafsi. Zahanati zipo 185, kati ya hizo za Serikali ni 148 na Binafsi ni 37 (Binafsi zitoazo huduma kwa faida ni 21, Mashirika ya Dini 10) na mashirika ya umma 6.
Huduma za kibingwa katika Mkoa.
Mkoa wa Manyara una hospitali mbili za rufaa katika ngazi ya Mkoa ambazo ni; Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Manyara yenye madaktari bingwa watano (5) na Hospitali ya Kilutheri ya Haydom yenye madaktari bingwa (8). Huduma za kibingwa zinazotolewa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa ni pamoja na
Upasuaji, afya uzazi na wanawake, magonjwa ya ndani. Aidha huduma zingine za kibingwa (watoto na mfumo wa mkojo) zinapatikana katika Hospitali ya Kilutheri ya Haydom.
Chanjo
Mkoa unatoa chanjo kwa watoto walio chini ya miaka mitano ili kuwapatia kinga dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo. Lengo likiwa ni kuhakikisha kiwango cha walengwa wa kupatiwa chanjo kinabaki kuwa zaidi ya asilimia 95 kwa watoto na akinamama. Chanjo zinazotolewa ni pamoja na chanjo ya kuzuia Kifua kikuu, Donda koo, Kifaduro, Pepopunda kwa watoto wachanga, homa ya ini na Kichomi. Chanjo nyingine ni ya kuzuia kupooza (Polio), Surua Rubela, chanjo ya kuzuia kichomi na kuharisha.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.