Na, Ruth Kyelula, Manyara RS
Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Manyara,ambazo ni Mbulu vijijini, Mbulu mji, Kiteto,Hanang’, Simanjiro, Babati vijijini na Babati mji, wamehimizwa kuendelea kusimamia kwa bidi utekelezaji wa afua za lishe ili kupunguza udumavu, ukondefu na utapiamlo.

Mkoa wa Manyara umeendelea kusimamia utekelezaji wa hali ya lishe na utoaji wa huduma za lishe kwa kupunguza vifo vya watoto na wajawazito.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga aliyasema hayo katika Mkutano wa Tathimini ya utekelezaji wa mkataba wa Afua za Lishe Julai 2024 hadi Juni 2025, uliofanyika katika jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa,Wilayani Babati Septemba 12, 2025.

Alisema ameridhishwa na kazi kubwa iliyofanyika katika kipindi cha mwaka mmoja (Julai 2024 – Juni 2025) ya kuendelea kusimamia mikataba ya lishe kikamilifu kupitia wakurugenzi wa Halmashauri hizo kwa kutenga fedha za kutatua changamoto mbalimbali.


Mhe. Mkuu wa Mkoa, alisema idadi ya watoto wenye ukondefu imepungua kutoka mwaka 2023/24 ambapo kulikuwa na watoto 21,603 hadi kufikia 2,324 pekee mwaka huu.

“Tumeokoa watoto takribani Zaidi ya 2,000 wamesalimika na utapiamlo, lakini tumewaongezea uhai, nguvu ya Taifa na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa wazazi ya kuwahudumia watoto, kubwa zaidi pia Serikali kuokoa matumizi ya vifaa tiba na madawa ya kuwatunza watoto hao, alisema Sendiga.”

Aidha, alisisitiza watoto kuzaliwa kwa uzito unaohitajika, wanawake kuwahi kliniki pindi wanapogundua kuwa ni wajawazito, kupata elimu ya lishe bora na kuhakikisha wataalamu wa Lishe wanaandaa afua zitakazoleta mabadiliko chanya kwa jamii.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.