Wilaya ya Simanjiro ni kati ya Wilaya tano (5) zinazounda Mkoa wa Manyara, ilianzishwa mwaka 1993 ikigawanywa kutoka Wilaya ya Kiteto. Wilaya inapakana na Wilaya ya Monduli upande wa Kaskazini Magharibi; Arumeru, Hai na Moshi upande wa Kaskazini; Kiteto upande wa Kusini; Kondoa na Babati upande wa Magharibi; na Mwanga, Same, Kilindi na Korogwe upande wa Mashariki. Wilaya ina eneo lenye ukubwa wa jumla ya kilometa za mraba 20,591. Wilaya ya Simanjiro imejaliwa kuwa na madini ya vito na ni eneo pekee duniani lenye madini ya Tanzanite.
Jiografia na hali ya hewa ya Wilaya
Wilaya iko katika eneo la nyanda kame na mbuga, hupata mvua za wastani wa kati ya milimita 400 na 500 kwa mwaka. Wilaya ina vipindi viwili vya mvua ambavyo ni vuli na masika. Mvua za vuli hunyesha kuanzia mwezi Novemba hadi Desemba na masika hunyesha kuanzia mwezi Machi hadi Mei.
Utawala, idadi ya watu na pato la Mwananchi
Utawala
Wilaya ya Simanjiro ina Tarafa sita (6), Kata kumi na nane (18), Vijiji hamsini na sita (56) na Vitongoji mia mbili sabini na nane (278).
Idadi ya Watu
Kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Wilaya ilikuwa na jumla ya wakazi 178,693, kati yao Wanawake ni 89,718 na Wanaume ni 88,975. Kwa mwaka 2021 Wilaya ilikadiriwa kuwa na jumla ya wakazi 222,842 kati yao wanawake 113,649 na wanaume 109,193 ikiwa ni ukuaji wa asilimia 3.2 kwa mwaka.
Hali ya Uchumi
Pato la Mkazi (D-GDP) kwa mwaka 2010 lilikadiriwa kuwa shilingi 268,000 na sasa linakadiriwa kufikia Shilingi 478,375 ikiwa ni ongezeko la asilimia 56.02. Shughuli kuu zinazowapatia kipato wakazi wa Simanjiro ni pamoja na Ufugaji (80%), Kilimo, Uchimbaji wa Madini, Uvuvi, Utalii na Viwanda vidogo vidogo (20%).
Fursa za Uwekezaji katika Wilaya ya Simanjiro
Serikali katika Wilaya ya Simanjiro imejielekeza katika kuendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ya kijamii ili kukuza mazingira wezeshi ya uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa wananchi kama vile uboreshaji wa vituo vya afya, zahanati na Hospitali ya Wilaya, kuanzishwa kwa miradi ya maji katika Vijiji na miradi mikubwa ya maji katika Miji midogo ya Orkesumet na Mirerani, ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya barabara, Usambazaji wa umeme Vijijini kupitia mradi wa REA awamu ya tatu na uanzishwaji wa ujenzi wa mradi mkakati wa Mji wa kimadini (Mirerani Tanzanite City). Maboresho haya yanazidi kuyafanya mazingira ya uwekezaji kuwa rafiki zaidi kwa wajasiriamali na wawekezaji wakubwa, wa kati na wadogo.
Wilaya ina ekari 1,500,000 zifaazo kwa kilimo cha mazao ya biashara na chakula. Kati ya hizo, takribani ekari 395,000 sawa na asilimia 26.3 hutumika kwa kilimo cha mazao ya chakula na biashara. Wilaya ina miundombinu ya umwagiliaji katika vijiji 8 ambavyo ni Ngage, Lemkuna, Kambi ya Chokaa, Gunge, Shambarai, Loiborsoit B, Londoto na Kiruani.
Wilaya ina mtandao wa Barabara upatao km 1971.71. Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) unahudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya km 603.1 katika Wilaya ya Simanjiro, kati ya hizo km 16.7 ni za lami na km 586.4 ni za changarawe. Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) anahudumia mtandao wa Barabara upatao km 1368.61. Barabara zinazohudumiwa na TARURA umegawanyika katika makundi 2 ambayo ni Barabara Ujazio (Feeder Roads) km 632.57 na Barabara za jamii (Community Roads) km 736.04.
Elimu.
Wilaya ina shule za msingi 99, kati ya hizo za serikali ni 84 na zisizo za serikali ni 15. Wilaya ina Shule za sekondari 19, kati ya hizo za serikali ni 16 na zisizo za serikali ni 3.
Wilaya ina Hospitali mbili, moja inayomilikiwa na serikali na moja inamilikiwa na kanisa la KKKT. Vituo vya afya vipo 4, kati ya hivyo 3 vinamilikiwa na serikali na 1 kinamilikiwa na shirika la dini. Wilaya ina jumla ya Zahanati 45, kati yake 38 zinamilikiwa na serikali, 5 zinamilikiwa na mashirika ya dini, 1 inamilikiwa na watu binafsi na 1 inamilikiwa na Taasisi ya Umma (TANESCO).
MADINI
Sekta ya madini ya Tanzanite ni miongoni wa sekta muhimu sana katika ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Simanjiro pamoja na uchangiaji pato la Taifa ambapo kutokana na umuhimu wake Serikali ilijenga ukuta wenye urefu wa km 24.5 ili kuyalinda ipasavyo madini haya adhimu, kipekee na dawamu duniani. Kuanzia tarehe 15.10.2021 vibali vya kusafirisha Madini ya Tanzanite nje ya Nchi (export permit) vilianza kutolewa Ofisi ya Madini Mirerani.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.