Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameipa siku tano za kazi kuanzia tarehe 26.10.2018 Wakala ya Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) kukamilisha kazi iliyosalia ya kufanya majaribio ya pampu katika mradi wa maji wa Mirerani, wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara.
Waziri Aweso ametoa maelekezo hayo kwa DDCA baada ya kukagua mradi wa maji wa Mirerani na kubaini kazi nyingine zimesimama kwasababu DDCA iliyofanya kazi ya uchimbaji haijatimiza jukumu lake la majaribio ya pampu kuwezesha kujua kiasi cha maji na kupima ubora wake kabla ya wananchi kupewa huduma hiyo.
Mh. Aweso amesema anataka mradi huo ukamilike ndani ya miezi sita, na baada ya majaribio ya pampu ameitaka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Babati (BAWASA) kufanya kazi ya usanifu wa mradi ndani ya siku saba. Hata hivyo, ametahadharisha mkandarasi atakayepewa kandarasi awe mwenye uwezo na uzoefu kwaniwananchi wamesubiri mradi huo kwa muda mrefu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa BAWASA Mhandisi Iddy Msuya amesema wako tayari kwa kazi hiyo, hata hivyo ameomba kutatuliwa changamoto ya kukosekana kwa gharama za usimamizi wa miradi hali iliyosababisha malalamiko na kutaka kushtakiwa na baadhi ya wazabuni. Amesema BAWASA inasimamia ujenzi wa miradi ya maji katika miji ya Mirerani, Orkesumet, Mbulu na Katesh.
Waziri Aweso (Mb) amesema changamoto zote zilizowasilishwa zitafanyiwa kazi haraka, kwasababu lengo ni moja la kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama karibu na makazi yao.
(Kwa picha mbalimbali na Video angalia sehemu ya Kituo cha Habari kisha nenda Maktaba ya Picha na Maktaba ya Video)
Imeandikwa Na: Haji A. Msovu
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.