Wakazi wa Halmashauri ya Mji wa Babati wametakiwa kuchangamkia fursa ya kujipatia mikopo ya asilimia kumi isiyo na riba kutoka Serikalini ili kuweza kujifanyia shughuli zao na kujikwamua na umaskini.
Hayo yamesemwa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Babati Bi. Amina Masood wakati wa ukaguzi uliofanywa na wataalam kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa wa kuangalia namna gani asilimia kumi zinazotokana na mapato ya ndani kama zinawafikia wananchi kama serikali ilivyoagiza.
"Sisi Halmashauri ya Mji wa Babati tumetenga Milioni themanini kwa ajili ya vikundi vya wanawake,Vijana na Walemavu lakini mpaka sasa kati ya vikundi kuna vikundi viwili tu vilivyokidhi masharti ya uchukuaji wa mikopo hiyo, hivyo nawasihi wananchi wa babati mjini kuunda vikundi na kuja Halamashauri ili kujipatia mikopo ya serikali kwani mikopo hiyo haina riba” Alisema Bi. Amina Masood.
Akizungumzia mikakati mbalimbali iliyowekwa na Halmashuari ili kuhakikisha wanawake,vijana na walemavu wa Babati wanaunda vikundi na kujitokeza kwa wingi kuomba mikopo hiyo Bi. Amina amesema kuwa wao kama Idara ya Maendeleo ya jamii imeweka Afisa Maendeleo ya Jamii kila kata ili wananchi wapate elimu juu ya uundaji wa vikundi na hatimaye waweze kupata mikopo hiyo.
Kwa upande wake Afisa Mipango wa Halmashauri ya Mji wa Babati Bw. Khamis Katimba amesema kuwa ili kuhakikisha kiwango cha fedha kinaongezeka kwa ajili ya kutoa asilimia kumi wao wamejipanga kuongeza vyanzo vya mapato katika Halmashauri na kuzuia mianya yote ya wanaokwepa kulipa kodi zinazotozwa na Halmashauri.
“Tutajitahidi kuongeza vyanzo vyetu vya mapato na kuziba mianya yote ya wakwepaji wa kodi za Halmashauri ili kuongeza makusanyo kwani tukiongeza makusanyo hata ile asimia kumi inayotakiwa kwa wanawake,vijana na walemavu itaongezeka”Alisema Mchumi huyo.
Pamoja na kuwataka wananchi hao kujiunga kwenye vikundi na kwenda Halmashauri kuomba mikopo hiyo vilevile Mchumi huyo alielezea changamoto mbalimbali za zinazojitokeza kwenye mikopo hiyo ikiwemo ya wananchi kudhani kuwa mikopo hiyo ni misaada na hivyo hawapaswi kurejesha na baadhi ya wanavikundi kukimbia ili wasilipe mikopo hiyo.
Akitoa ufafanuzi juu ya dhana ya wananchi kudhani kuwa hawapaswi kurudisha mikopo hiyo Afisa Usimamizi fedha kutoka TAMISEMI Bwana Ismail Chami alisema kuwa lazima wananchi hao wapewe elimu ili kujua kuwa fedha hizo sio sadaka bali ni mikopo ya kuwafanya wajikwamue kutokana na umasikini ndo maana Serikali inatoa bila riba yoyote.
"Maafisa Maendeleo ya Jamii lazima mkatoe elimu juu ya mikopo hii na wananchi wafahamu kuwa nia ya serikali ni kuwasaidia wananchi wake ndo maana mikopo inatolewa kwa wanawake,vijana na walemavu bila riba yoyote hivyo lazima mikopo hiyo irejeshwe ili wengine waweze kukopa" Alisisitiza Bwana Chami.
Maafisa hao kutoka TAMISEMI pia walipata nafasi ya kwenda kuvitembelea Kikundi cha Mrawa kilichopo Mrara kinachojishughulisha na usindikaji wa nafaka,Viungo vya chai na pilipili, Kikundi cha KIBATIMA kilichopo Mtaa wa Nyunguu kinachojishughulisha na uuzaji wa Mabatiki ili kujionea jinsi walivyotumia mikopo hiyo ya serikali kujianzishia miradi ya maendeleo na kujiingizia kipato na kuwataka Maafisa Biashara wa ngazi ya Halmasahuri kuwatafutia masoko ili wapate kuuza bidhaa zao na waweze kufanya marejesho kwa urahisi.
"Ningependa kuwaambia wana vikundi washirikiane na wataalam wa Halmashauri ili watanue soko na kufikia malengo"Alisema Bwana Fulgence Matemele Mchumi kutoka TAMISEMI.
Serikali imeweka sheria kwa kila Halmashauri kutenga asilimia kumi (asilimia nne kwa wanawake,asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa walemavu) kutokana na mapato ya ndani na kuwapa mikopo isiyo na riba ili kuwawezesha kuanzisha miradi na kujikwamua kiuchumi.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.