Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) jana tarehe 13 Machi, 2020 ilifanya ziara katika Halmashauri ya Mji wa Babati Mkoani Manyara kwa kutembelea miradi ya Ujenzi wa Barabara za lami na Standi Mpya ya Mabasi ya Babati.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati Bw. Fortunatus Fwema ( wa kwanza kulia) akiiongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) kukagua barabara za lami mjini Babati.
Wabunge hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Mh. Vedasto Ngombale Mwiru aliisifia Halmashauri ya Mji wa Babati kwa ujenzi mzuri wa barabara za lami katika mitaa ya Babati kwani Barabara na taa zilizojengwa zinapendezesha mji na kuonekana na mandhari ya kuvutia ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mitaro ya kupitisha maji na upandaji wa miti pembezoni mwa barabara.
Sehemu ya barabara ya lami iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Babati.
“Kwa kweli tumefurahishwa na ujenzi wa Barabara za lami katika Mji wa Babati na tungependa Halmashauri zingine kuja kujifunza kwa hapa” Aliongeza Mwenyekiti wa Kamati.
Pia walizitaka Halmashauri nyingine nchini zenye miradi kama hiyo kuja kujifunza katika Halmashauri ya Mji wa Babati.
Pamoja na kupongeza ujenzi wa Barabara hizo Wabunge hao walishauri wakati wa ujenzi kuongeza upana wa mitaro ili kujihadhari na mafuriko na pia kuweka sharia ndogondogo zitakazoweza kuzilinda barabara hizo kudumu kwa muda mrefu.
Baada ya kumaliza ukaguzi wa barabara za lami wajumbe wa kamati hiyo pia walitembelea Stand mpya ya Mabasi iliyopo katika eneo la Maisaka katani na kujionea maendeleo katika Stand hiyo.
Akitoa maelezo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati Bw. Fortunatus Fwema alisema katika eneo hilo kutakuwa na stand ya mabasi, magari ya mizigo, magari madogo,eneo na magari ya kusubiria abiria pamoja na sehemu za huduma za kifedha ili kuwarahisishia wasafiri na watumiaji wa eneo hilo huduma za uhakika.
Sehemu ya stand Mpya ya Mabasi iliyotembelewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC)
Akitoa malalamiko yake mbele ya Kamati hiyo Mfanyabiashara katika eneo hilo la stand alisema kuwa tatizo ni kuwa Halmashauri imewapa maeneo yenye vipimo vidogo na hivyo kushindwa kupanua biashara zao na pia kuna changamoto ya eneo la kupunzikia hasa wakati wa mvua kwani eneo lililopo ni dogo mno.
Akiongea wakati wa majumuisho ya ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati Mheshimiwa Vedasto Kingunge alitoa maelekezo kwa Halmashauri kuahakikisha inaongeza ukubwa wa eneo la vibanda na kujenga sehemu nyingi za kupunzikia wasafiri na wafanyabiashara katika eneo hilo.
“Halmashauri hakikisheni mnaongeza ukubwa wa eneo la vibanda vya biashara na kujenga sehemu za kupunzikia ili wanufaika na stand wakae mahali salama na vilevile fanyeni haraka kumalizia stand hii itasaidia kuongeza mapato ya Halmshauri yenu na kuliongezea thamani eneo mlilopima viwanja” Alisongeza Mwenyekiti huyo.
Halmashauri iliamua kuhamishia Stand katika eneo hilo kutoka Mjini ilipokuwa stand ya zamani mara baada ya Chama Cha Mapinduzi kuchukua eneo lao.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.