Na Nyeneu, P. R - Dareda
Waziri wa ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa amemuagiza mtendaji mkuu wa wakala wa Barabara kuu nchini (TANROADS) kuhakikisha hawawafumbii macho wakandarasi wanaoshindwa kufanya kazi kwa wakati wanazopewa na serikali na kukwamisha mipango ya serikali ya kuhakikisha kila mkoa unakuwa na barabara zenye viwango.
Bashungwa ameyasema hayo leo katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Dareda – Dongobesh (Kilomita 60) sehemu ya Dareda Center - Dareda Mission yenye urefu wa kilomita 7. Amesema ujenzi huo ni utekelezaji wa ahadi ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wananchi wa mkoa Manyara wa kukarabati barabara korofi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga amesema hafla hii ilipangwa kufanyika Disemba mwaka 2023 na iliahirishwa kutokana na maafa yaliyotokana na maporomoko ya matope yaliyotokea Wilayani Hanang ambapo amemshukuru Mhe. Waziri Bashungwa yeye na timu yake kwa kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na maporomoko hayo.
Pia Mhe. Sendiga amesema Barabara hiyo inaunganisha Wilaya mbili ambazo ni Wilaya ya Mbulu na Wilaya ya Babati ambapo ameitaka mamlaka husika kuhakikisha wakati ujenzi unaendelea wananchi wa maeneo hayo wawe wanufaika wa mradi huo kwa kupata ajira ndogondogo wakiwemo mama ntilie kwa ajili ya kuwapikia chakula wakandarasi.
Nae mtendaji mkuu wa TANROADS nchini Mohamed Besta amesema mradi huo utaghalimu kiasi cha shilingi bilioni 9.88 ambapo amemuagiza mkandarasi anaesimamia mradi huo kufanya kazi kwa weledi na kukamilisha kwa muda uliopangwa.
Aidha, Mbunge wa jimbo la Babati Vijijini ambae pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya ndani Mhe. Daniel Sirro amesema ni kwa muda mrefu wananchi wa Dareda wamekuwa wakilalamikia barabara hiyo, hivyo ujenzi wa barabara hiyo utasaidia kuuunganisha mawasiliano katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa manyara na kukuza uchumi kwa wananchi.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.