Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga leo Feb 27, 2024 amezindua Ofisi ya Shirikisho la Wamachinga na Bodaboda iliyojengwa mjini Babati. Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema, uwepo wa ofisi hii ni maono ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kwamba kila kundi lazima lifikiwe na litengenezewe mazingira mazuri ya kufanya kazi ili waweze kuwa wazalishaji wazuri.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema ofisi hiyo iliyojengwa kwa thamani ya zaidi ya shilingi milioni 43, ikiwa na umeme, maji pamoja na samani ambapo fedha hizo ni kutoka serikali kuu, mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na michango ya wadau mbalimbali itakuwa ni mahsusi kwa makundi hayo katika kufanya vikao, mijadala na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Vilevile RC Sendiga amewataka Wamachinga pamoja na Bodaboda kutojichukulia poa kwani wao ni watu muhimu katika kusaidia upatikanaji wa kodi ambayo inakwenda katika shughuli mbalimbali za kiuchumi katika nchi yao, kwani serikali inategemea kodi katika uboreshaji wa huduma za Afya, Elimu, Maji, Miundombinu n.k. “Kwahiyo hapo ulipo jipigepige kifuani sema kuanzia leo sijichukulii poa”. Aliongeza mkuu wa Mkoa.
Kabla ya kufanya ufunguzi wa ofisi hiyo, RC Sendiga amemuahidi Mkuu wa Wilaya ya Babati Mhe. Lazaro Twange kuwa ataleta Kompyuta mbili katika ofisi hiyo ya wamachinga na Boda Boda ili kuwawezesha kufanya Biashara zao kidijitali. “Muwaangalie wafanyabiashara wadogo wadogo wa China, India wanafanyaje Biashara zao”. Aliongezea Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Mkuu wa mkoa ametembelea na shule ya sekondari Kololi iliyopo Katika Kata ya Maisaka na Pauline Gekul iliyopo katika Kata ya Bonga kuona mwenendo wa ukamilishaji wa baadhi ya Majengo ya shule hizo na kutoa maagizo ya ukamilishwaji wa haraka kwa majengo hayo ambayo baadhi ni vyoo vya wanafunzi, majengo ya Maabara za TEHAMA.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.