Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alisema kuwa chaneli mpya ya utalii inatarajiwa kuvutia watalii wengi zaidi kuja nchini sambamba na kuongeza pato la taifa.
Akizungumza tarehe 15 Disemba jijini Dar es salaam, alipokuwa akizindua chaneli hiyo ya utalii inayojulikana kama “Tanzania Safari channel” Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alisema kuwa chaneli hiyo mpya itatoa fursa ya kutangaza wanyama mbalimbali waliopo katika hifadhi za wanyama, utamaduni wa watanzania pamoja na vivutio mbalimbali vilivyopo nchini ili kuvutia watu wengi zaidi kuja kufanya utalii na hatimaye kuongeza kiasi cha fedha kitachochangia katika pato la taifa.
“Chaneli hii ni njia muhimu ya kutangaza utalii ndani na nje ya nchi yetu, ambapo itaongeza idadi ya watu watakaotembelea Tanzania” alisema Waziri Mkuu Majaliwa
Waziri Mkuu Majaliwa aliongeza kuwa kwa sasa watalii wanaokuja nchini kwa mwaka ni milioni 1.3 , na matarajio ya Serikali ni kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni 2 ifikapo mwaka 2020, hivyo chaneli hiyo ya utalii itasaidia katika kufikia lengo hilo la Serikali.
Naye, Waziri Utalii na Maliasili Dkt. Khamis Kigwangala alisema kuwa sekta ya utalii nchini inachangia asilimia 17.7 katika pato la taifa, na katika mwaka 2017 shilingi trilioni 5.04 zilipatikana kupitia sekta hiyo, na hivyo Serikali imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali itakayo saidia kukuza utalii na kuongeza pato la taifa
Akitolea mfano mikakati hiyo kuwa ni “kuimarisha masoko ambapo wataalamu wa utalii wameshafanya maonesho ya barabarani katika baadhi ya nchi na hivi karibuni watafanya maonesho hayo nchini China ili kuongeza masoko mapya” alisema Waziri Kigwangala
Waziri huyo wa Maliasili na Utalii, alifafanua mikakati mingine ya wizara hiyo ni kuweka mabango yenye picha mbalimbali za vivutio vya utalii katika barabara inayoelekea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Aidha, Waziri huyo ametoa fursa kwa wasanii mbalimbali wakiwemo wa filamu na muziki kutumia sehemu za vivutio vya utalii nchini kwa ajili ya kutengeneza kazi zao za sanaa.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, kutoka Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Dkt. Saleh Yusuph Mnemo alisema kuwa chaneli hiyo inatarajiwa kuwasaidia watu wengi kufahamu vivutio vya utali vilivyopo nchini sambamba na kuongeza mapato, ambapo Zanzibar peke yake ina vivutio vya mambo ya kale 39.
Naibu Katibu Mkuu huyo, alifafanua kuwa asilimia 80 ya fedha za kigeni zinazopatikana Zanzibar zinatokana na sekta hiyo, huku ikichangia asilimia 20 katika pato lake la taifa.
Chaneli hiyo ya utalii inayojulikana kama Tanzania Safari Channel inaonekana kupitia kisimbuzi cha Startimes namba 331, na kurusha matangazo yake kwa lugha mbalimbali
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.