Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga amekuwa mgeni rasmi katika kikao kazi na wadau wa mbegu za mazao kilichoandaliwa na Tume ya ushindani Kanda ya Kaskazini.
Kikao kazi hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuwahusisha wadau mbalimbali wakiwemo wakulima, wauzaji wa mbegu za mazao, maafisa ugani kilikuwa na lengo la kujadili hali ya ushindani wa kibiashara katika upatikanaji, uzalishaji na usambazaji wa mbegu za mazao nchini.
Aidha, katika hotuba yake Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema kuwa ili biashara iweze kuwa na tija ni lazima ifanywe kwa kufuata taratibu, miongozo kanuni na sheria zilizowekwa. Vilevile aamewatahadharisha wafanyabiashara juu ya vitendo viovu vinavyo fifisha ushindani katika biashara kama vile kupanga bei moja, kupanga na kuzalisha aina moja ya bidhaa n.k.
“Ni lazima kila mwenye biashara awe na kitu chake, awe na bei zake lakini kwa kufuata sheria, kanuni, miongozo na taratibu ili kuleta ushindani” akisisitiza Mhe. Mkuu wa Mkoa.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema serikali awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan imekuwa kinara katika kuinua sekta ya kilimo na wakulima kupitia uanzishwaji wa viwanda vidogo na vikubwa vya uzalishaji na kuweka mazingira ya amani kwa wafanyabiashara.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.