Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Joel N. Bendera akishirikiana na Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro Mhe. Anna Mghwira wameongoza kikao cha ujirani mwema cha kujadili hatua waliyofikia kulinda Mazingira na viumbe hai hasa samaki katika Bwawa la Nyumba ya Mungu lililofungwa mwezi Mei 2016 ili kuzuia uvuvi haramu na kuruhusu samaki kuzaliana katika Bwawa hilo.
Aidha, baada ya Kikao hicho kilichofanyika Mkoani Kilimanjaro katika ukumbi wa Mikutano wa Wilaya ya Mwanga, ujulikanao kama Teachers Learning Centre na kujumuisha Kamati za Ulinzi na Usalama za pande zote mbili, wataalamu mbalimbali na baadhi ya wajumbe kutoka Wilaya ya Simanjiro na mwanga,Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa walikwenda kuongea na wananchi wa kijiji cha nyumba ya Mungu kata ya Ngorika Wilaya ya Simanjiro ambapo Mheshimiwa Dkt.Bendera alifungua rasmi Bwawa hilo na kuwataka wananchi wa Kijiji hicho kuzingatia maagizo yote ya matumizi ya Bwawa hilo.
Mheshimiwa Dkt.Bendera amesisitiza kuwa kutokana na makubaliano ya kikao cha awali kabla ya Mkutano na wananchi Bwawa hilo litakuwa likifungwa tarehe moja Januari kila mwaka hadi tarehe 30.6 kila mwaka ili kuruhusu samaki kuzaliana.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.