Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Joseph Mkirikiti amemuagiza Meneja wa Tanesco Wilaya ya Kiteto Mhandisi Lazaro Lenoy kuhakikisha anatatua kero za upatikanaji wa umeme katika wilaya hiyo ili wananchi waweze kujipatia huduma muhimu ikiwemo upatikanaji wa maji.
Mhe.Mkirikiti ameyasema hayo jana alipokuwa akikagua miradi ya maji inayosimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Kiteto.
“Tatizo la umeme katika wilaya ya Kiteto limesababisha wananchi wetu kukosa huduma muhimu ikiwe maji, kwa hiyo nawaagiza Tanesco Kiteto kumaliza hizi kero za upatikanaji wa umeme ili RUWASA ipeleke maji kwa wananchi hawa kwa urahisi” Alisema Mhe.Mkirikiti
Akielezea jinsi RUWASA inavyotekeleza miradi ya maji wilayani humo Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Kiteto Mhandisi Stephano Mbaruku amesema kuwa RUWASA mwaka 2021 inakusudia kuwapelekea maji wakazi 275,916 ukilinganisha na wakazi 92,080 ya mwaka 2019 na hadi kufikia mwaka 2023 inatarajiwa kuwafikia wakazi wa vijiji 28 vilivyobaki.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa RUWASA Wilaya ya Kiteto imepokea shilingi 169,346,810 kwa ajili ya kumalizia utekelezaji wa kazi za ujenzi wa miradi ya maji ya wezamtima na Ostet na miradi hii ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ili huduma ya maji ipatikane kama ilivyokusudiwa” Alisema Mhandisi Mbaraku.
Pamoja na Miradi ya maji ya Wezamtima na Ostet RUWASA wilayani Kiteto pia imetekeleza miradi ya maji ya Matui wenye gharama 692,918,911, mradi wa Mdinku wenye gharama ya shilingi 168,108,923.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Pamoja na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa wananchi wa Kiteto lakini kuna changamoto ya kutokuwepo au kukatika mara kwa mara kwa nishati ya umeme hali inayopelekea mashine za Kusuma maji kushindwa kufanya kazi” Aliongeza Mhandi huyo wa RUWASA Wilaya ya Kiteto.
Kwa upande wake Mjumbe wa kamati ya siasa Mkoa wa Manyara ambaye ni Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Manyara Bwana Jacob Siay ameonesha kuridhishwa na jinsi RUWASA inavyotekeleza Ilani ya Chama kwa kuhakikisha wananchi katika Vijiji vyote wanapata huduma ya maji safi na salama na kuwashauri wananchi wa Mkoa huo kuhakikisha wanatunza miundombinu ya maji.
“Kiukweli sisi kama kama kamati ya Siasa ya Mkoa wa Manyara tumeridhishwa na jinsi RUWASA inavyotekeleza miradi ya maji na sisi tunataka kuona ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inatekelezwa katika sekta mbalimbali” Alisisitiza Bwana Jacob Siay.
Katika Wilaya ya Kiteto Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mheshimiwa Joseph Mkirikiti akiambatana na Kamati ya Siasa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa huo bwana Musa Missaile wamekagua miradi minne kati ya miradi nane inayotekelezwa na RUWASA kwa mwaka 2021.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.