Ikiwa zimebaki siku 6 kuelekea uchaguzi mkuu nchini kamati ya maridhiano na baraza la wazee Mkoa wa Manyara limewataka wananchi kuepuka maneno ya uchochezi na yenye kuleta mgawanyiko katika Taifa ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya wanasiasa ili kuepusha uvunjifu wa amani na umoja wa taifa.
msisitizo huo wa kudumishwa kwa amani na umoja wa kitaifa umetolewa leo na kamati ya amani kwa kushirikiana na Kamati ya wazee wa Mkoa wa Manyara kwa lengo la kupinga kauli iliyotolewa hivi karibuni na kiongozi wa taasisi ya kiislam na kueleza kuwa kauli hiyo ni kauli ya kuleta mgawanyiko licha ya kukiri kuwa haina ukweli juu ya makubaliano yaliyotajwa.
"kuna jambo moja limejitokeza kwa baadhi ya wagombea wakisema kuwa viongozi wa dini tumeelekeza kuwa kura zipigwe upande gani,jambo hilo siyo sahihi kuna mtu ametangaza waislamu tumekaa na kuamua kura zipigwe kwa nani ,sisi waislamu kwa ujumla hakuna kikao kilichokaa"alisema mwenyekiti wa kamati hiyo Juma Mkola.
aidha mwenyekiti wa kamati hiyo alieleza kuwa kiongozi mkuu wa waislamu ni mufti wa Tanzania na kwamba hakuna kikao kilichokaliwa na kufikia muafaka wa kuunga mkono upande wa chama chochote kwa kuwapigia kura .
"sisi kama kamati ya maridhiano kazi yetu ni kusisitiza amani na utulivu watanzania hatujazoea vurugu watanzania ni watu wa amani kwenye misikiti kwenye makanisa sisi kazi yetu ni kutangaza amani na siyo kuelekeza vitu vilivyo kinyume na utaratibu wa amani nchi yetu toka tupate uhuru ni amani "alisema Mkola.
Naye katibu wa wazee Mkoa wa Manyara Aurelia Asenga alisema kuwa ni wakati wa wazee kusimama katika nafasi zao sawasawa ili waweze kuwaweka vizuri vijana na watu wengine wanaotaka kuipotosha amani katika taifa.
alisema amani ikipotea katika taifa wanaoumia wengi ni kinamama ,watoto ,wazee na walemavu ni hiyo ni kwasababu hata ikitokea vita makundi hayo hayawezi kukimbia.
"vijana watatudang'anya twende huku mara vile kwasababu tu wao wananguvu zao lakini tukiwafatilia sisi tutapotea hivyo ni wajibu wetu wazee kusimama katika eneo letu kwa kuwaelimisha hawa vijana,watoto na wazee wenzetu"alisema Aurelia.
Naye Makamu Mwenyekiti wa kamati ya mardhiano Askofu Eliya Dahhi alisema wanasisitiza amani kutokana na athari zinazojitokeza pale amani inapokosekana kwani hakuna kitakachofanyika endapo amani itatoweka.
kuhusu uchaguzi siku ya oktoba 28 kamati hiyo imewasihi wananchi wote wenye sifa kujitokeza kupiga kura huku wakisisitiza wananchi hao kuondoka katika eneo la kupiga kura na kusubiri matokeo wakiwa nyumbani.
"wasishawishiwe kama wanavyoshawishiwa na vyama vingine kwamba baada ya kumaliza kupiga kura wabaki wakisubiri matokeo vituoni"waliongeza.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.