Na Nyeneu, P. R - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Kwa mwaka wa fedha 2023-2024, TARURA Mkoa wa Manyara imetengewa Bajeti ya kazi za matengenezo ya barabara, miradi ya maendeleo, shughuli za utawala na usimamizi wa miradi kwa ujumla wa Shilingi 20,716,671,301.98. Hayo yamesemwa na Mhandisi Magiri Kaimu Meneja TARURA Mkoa wa Manyara wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ujenzi na matengenezo ya barabara kwenye kikao cha kwanza cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Manyara kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga Novemba 28, 2023 katika ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Aidha, kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, TARURA Mkoa wa Manyara imepanga kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ujumla wa barabara za lami km 11.20, barabara za changarawe km 251.67, ujenzi wa madaraja mapya 26, kalivati 7, mitaro ya maji ya mawe na zege mita 1,920 kwa makisio ya Shilingi 14,550,000,000 Pia, Wakala hiyo imepanga kuweka taa za mwanga barabarani 241 kwa Shilingi 1,077,740,000 katika Wilaya za Babati, Hanang’, Mbulu, Kiteto na Simanjiro.
Vilevile Mhandisi Magiri ameeleza kuwa pamoja na kazi zote, Wakala inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uharibifu wa miundombinu hasa mifereji, kung’olewa kwa alama za barabarani na uvamizi wa hifadhi ya barabara kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Wakala wa Barabara za Vjijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Manyara inasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 6,759.726. Kati ya hizo kilomita 2,314.993 ni Barabara unganishi (Collector Road), kilomita 3,209.638 ni Barabara ujazio (Feeder Road) na kilomita 1,235.095 ni Barabara Jamii (Community Road). Barabara za lami ni kilomita 30.634, barabara za changarawe ni kilomita 1,558.858 na barabara za udongo ni kilomita 5,170.234.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.