Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi Bilioni 29.9 kukamilisha ujenzi wa maboma ya shule za sekondari yapatayo 2,392 nchini ili kuwawezesha wanafunzi wote kuweza kujiunga na elimu ya sekondari katika mwaka 2019.
Akiongea katika ziara yake ya kikazi mkoani Manyara katika shule ya sekondari Nangara na Kwaangw zilizopo Halmashauri ya Manyara Mji Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema Serikali imejipanga katika kuahakikisha mpango wake wa kuwapatia elimu ya sekondari watoto wa Kitanzania inakamilika na hivyo imehakikisha maboma yote ya shule za sekondari yanakamilika kwa wakati na kuanza kutumika kabla ya mwishoni mwa mwezi Juni,mwaka huu.
Amewataka watendaji wote kuongeza kasi ya kusimamia ujenzi wa maboma hayo na kwamba yanakamilika kwa fedha zilizopangwa na kwa ubora unaotakiwa.
Aidha, Nyamhanga amesema Mkoawa Manyara una maboma 139 ambayo baadhi yamekamilika nay ale ambayo bado amemtaka Katibu Tawala Mkoa Manyara Bw. Mussa Masaile na timu yake kusimamia kikamilifu ujenzi huo ikiwa ni pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa mingine nchini.
Vilevile amesema Serikali inapeleka fedha mashuleni shilingi Bilioni 28.5 kupitia Mpango wa Serikali wa Elimu Bila Malipoili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu bila kulipia kuanzia shule za awali, msingi hadi kidato cha nne kwa lengo la kumpatia elimu kila motto wa Kitanzania.
Aidha, amesema kiasi kingine cha fedha shilingi 35.2 Bilioni kitatolewa na Serikali katika mwezi huu ili kukamilisha maboma yote ambayo yamesalia.
Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari Babati Mji amesema katika mwaka 2019 hakuna aliyekosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza na wataendelea kusimamia miradi ya maendeleo ya sekta ya elimu ikiwemo ile ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R).
Mhandisi Nyamhanga anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Manyara kujionea utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, barabara, mikopo ya vikundi na utawala bora.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.