Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Bwana Musa Missaile amewaongoza Wakuu wa Wilaya wote wa Mkoa wa Manyara,Kamati ya Usalama ya MKoa na watumishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa kumpokea Mkuu wa Mkoa mpya wa Mkoa huo Mheshimiwa Makongoro Nyerere alipowasili rasmi leo Jumamosi kuanza kazi rasmi.
Baada ya mapokezi hayo Katibu Tawala alimuongoza Mheshimwa Makongoro kuelekea katika Ofisi yake na kupata taarifa fupi juu ya mazingira ya Mkoa.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa karibu sana Mkoani Manyara leo ni siku ya kukukaribisha tu ofisini lakini utapata muda wa kuongea siku ya jumanne katika shughuli rasmi ya makabidhiano ya Ofisi kati yako na Mwenyeji wako Mheshimiwa Joseph Mkirikiti aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa” Alisema Katibu Tawala.
Mara baada ya mapokezi hayo Mhe.Makongoro Nyerere alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Salimia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara na aliwashukuru viongozi wote Pamoja na watumishi waliojitokeza kumpokea na kuwaahidi kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa bila kukwazana kwa namna yoyote.
“Pamoja na nafasi mbalimbali nilizowahi kushika katika uongozi lazima niseme sijawahi kuwa Mkuu wa Mkoa, kwa hiyo nategemea kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwenu na nitakuwa mtu wa kushirikiana na nyinyi kila sehemu ili kuhakikisha tunawaletea wananchi wetu maendeleo” Alisema Mhe. Makongoro.
Mheshimiwa Makongoro Nyerere ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara kuchukua nafasi ya Mheshimiwa Joseph Mkirikiti aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.