Katibu Tawala Mkoa wa Manyara Bwana Missaile Musa amemtembelea kampuni ya XIN SI LU kutoka Kichana inayowekeza katika uzalishaji wa samaki katika Kijiji cha Shaurimoyo kata ya Kisangaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoani Manyara.
Akiawa katika ziara hiyo Katibu Tawala akiambatana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati Bwana. Hamisi Malinga alijionea hatua mbalimbali za ukuzaji wa samaki mpaka anapofikia hatua ya kufaa kuliwa.
Akitoa maelezo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Msimamizi wa Kampuni hiyo alisema kuwa Kampuni hiyo imeanza kazi kuanzia Mwezi wa sita 2019 na mpaka sasa imetoa ajira za muda kwa watanzania ishirini na wachina wane.
“ Kampuni yetu mpaka sasa imesaidia jamii kwa kusafisha sehemu ya barabara kwa kutumia katapila la kampuni wakati wa kipindi cha mafuriko kwa wakazi wa Kisangaji na pia tunatarajia kutoa ajira za kudumu nyingi zaidi mara ujenzi utakapokamilika” Alisisitiza Msimamizi huyo.
Akimkaribisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati Bwana Hamisi Malinga alisema kuwa ujenzi wa kampuni hiyo utasaidia kutoa ajira kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo na wengine kulingana na ujuzi walio nao na pia wananchi watapata ujuzi wa kufuga samaki na kuweza kuanzisha mabwawa ya samaki katika makazi yao na hivyo kuwaongezea kipato.
Mara baada ya kupata maelezo na kukagua mradi huo Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara aliwataka wawekezaji hao kuhakikisha wanafuata sheria za nchi na kujiepusha na uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuisadia jamii inayozunguka eneo hilo kwani utunzaji wa mazingira ni jukumu lao.
“Hakikisheni katika kipindi chote mtakachokuwa hapa mnafuata sheria za nchi yetu ikiwa na kuhakikisha wafanyakazi wote wasio watanzania wanakuwa na vibali vya kufanyia kazi, kutunza mazingira yanayolizunguka eneo hili pamoja na kuisadia jamii husika katika mambo ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kushiriki katika ujenzi wa shule, zahanati na shughuli nyingine za kijamii” Alisema Katibu Tawala.
Ujenzi wa mabwawa hayo ya samaki katika eneo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Tanzania ya viwanda ambayo itasaidia kuwezesha watanzania wengi kujikwamua na umasikini kwa kuajiriwa na wengine kujiajiri kwa kuangalia fursa mbalimbali zitakazopatina katika eneo hilo.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.