Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Bwana Missaile Musa akiambatana na Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Bwana Anza-amen Ndossa,Katibu wa Afya Mkoa Bwana Thomas Malle na Mjumbe wa Kamati ya Afya Mkoa Dkt. Peter Neema jana tarehe 28/11/2018 amefanya ziara ya kukagua ujenzi katika viytuo vya afya na mabweni ya wanafunzi wilayani Mbulu ili kuona maendeleo ya ujenzi huo unavyukwenda katika kuwaletea wananchi na wanafunzi huduma nzuri na za haraka.
Ziara ya Katibu Tawala ilianzia huko Dongobesh kwa kuangalia ujenzi wa Kituo cha Afya Dongobesh na kukuta ujenzi wa majengo ya Maabara,Wodi ya wazazi,jengo la kuhifadhia maiti,nyumba ya mtumishi na njia za kutembelea ukiendelea kwa kasi ndogo na kuiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kuharakisha ujenzi wa kituo hicho ikiwa na pamoja na kurekebisha kasoro ndogondogo zilizopo kwenye milango ili kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa mwezi Novemba wananchi wa Dongobesh waanze kupata huduma katika majengo hayo kama alivyoagiza Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa ziarani Mkoani Manyara.
Katika kituo cha afya Tlawi Katibu Tawala alikagua wodi za wagonjwa,njia za kutembelea,nyumba ya mtumishi pamoja na maabara na aliwakuta mafundi wakiendelea na hatua za mwisho za ujenzi na kuwataka wasimamizi wa kituo hicho kuanza kupanda miti na bustani kuanzia kipindi hiki cha mvua ili kituo cha Afya kiwe na mandhari ya kuvutia.
Baada ya kutoka katika kituo cha Afya Tlawi Katibu Tawala wa Mkoa alitembelea katika Shule ya Sekondari Chief Sarwatt ili kuangalia ujenzi wa mabweni mawili (moja la wasichana na moja la wavulana) na kumtaka Mkuu wa Shule hiyo kuongeza kasi ya kumalizia mabweni hayo ili kuhakikisha ifikapo Januari 2019 wanafunzi wote watakaopangiwa kujiunga na shule hiyo wanapata nafasi ya kusoma katika mazingiara mazuri.
Akiendelea na ziara yake katika kituo cha afya Daudi Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara aliridhishwa na hatua zilizofikiwa katika kituo hicho kwani ina vifaa vya kisasa na na majengo yamekamilika ila alishauri katika katika changamoto ya maji Mganga Mfawidhi wa kituo hicho ahakikishe Tanki la maji lililopo kituoni hapo litafutiwe namna ya kujengewa ili liwe juu kuwezesha maji kutiririka kwenye mabomba hasahasa Maabara.
Akihitimisha ziara yake katika Shule ya Sekondari Gehandu Katibu Tawala Mkoa alikagua ujenzi wa mabweni mawili na kuitaka kamati ya ujenzimkuharakisha ujenzi huo ili kuhakikisha wanafunzi wanapata sehemu salama ya kulala na kujifunzia.
Katibu Tawala wa Mkoa amekuwa akifanya ziara za mara kwa mara katika wilaya zote ili kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri zote zilipo Mkoani Manyara.
(Kwa picha mbalimbali na Video angalia sehemu ya Kituo cha Habari kisha nenda Maktaba ya Picha na Maktaba ya Video)
Imeandikwa Na: Haji A. Msovu
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.