Na Mwandishi wetu - Mjini Babati
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amehitimisha Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 Mkoani Manyara na kuhudhuria Misa Takatifu ya kumuombea Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Kanisa la Parokia ya Roho Mtakatifu lilipo Mjini Babati.
Pia Mhe. Rais amesisitiza kuziishi falsafa za Mwalimu Nyerere na kutozipuuza ikiwa ni pamoja na kudumisha Umoja ambayo ni moja ya falsafa ambazo Mwalimu Nyerere alihimiza katika maisha ya uhai wake. Ameongeza kuwa Serikali imeweka jitihada za kuboresha maisha ikiwemo ujenzi wa Vyuo ya VETA ambapo lengo ni kuwajengea Vijana hao ujuzi.
Vilevile Mhe. Rais amezikumbusha Halmashauri zote nchini na wananchi kupanda miti na kutochoma moto ovyo mashamba, kwani kufanya hivyo kuna sababisha mabadiliko ya tabia ya nchi. Pia, amezipongeza Taasisi zinazofanya kampeni juu ya upandaji miti na utunzaji wa mazingira. Mhe. Rais amesisitiza mashindano juu ya upandaji miti yaendelee ili kuhamasisha zoezi la upandaji miti na kutunza mazingira.
Mhe. Dk.Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi kuwashauri wananchi kuacha kilimo cha zao la bangi na kulima mazao ya biashara au kufanya shughuli zingine za kiuchumi tofauti na hizo za madawa ya kulevya kwani hakina tija na kinaleta madhara kwa Taifa. Sambamba na hilo amewataka wananchi kuchukua tahadhari kubwa juu ya ugonjwa wa Ukimwi, amesisitiza kuhusu umuhimu wa lishe huku akiwataka Wakuu wa Mikoa kulishughulikia suala hilo ili kupunguza na kuondoa changamoto ya udumavu.
Mwenge wa Uhuru 2023 wenye kaulimbiu “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe hai na Uchumi wa Taifa” umekimbizwa katika Mikoa 31 na Halmashauri 195 za Tanzania Bara na Visiwani kuhamasisha Amani, Umoja, Upendo na Mshikamano wa Kitaifa, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo ambapo Mwenge ulipita na kuwahimiza Wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
Picha na Nyeneu, P. R
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.