Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe.Joseph Mkirikiti amewataka wakulima wa mkoa huo kulima kilimo chenye tija na kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ili yaweze kuwanufaisha na kuongeza kipato cha mkulima wa mkoa wa Manyara.
Mhe. Mkirikiti ameyasema hayo leo mjini Babati alipokuwa akifungua kikao kazi cha mafunzo ya uhamasishaji wa matumizi bora ya zana za kilimo kwa wakulima wadogo na wakubwa kutoka wilaya ya Babati na Mbulu
“Tutambue kuwa sekta za kipaumbele za kiuchumi katika Mkoa wa Manyara ni kilimo,ufugaji,madini,utalii na biashara na ndio vyanzo vikuu vya mapato katika Mkoa wetu.Kwa kutambua umuhimu huo ni vyema kwa wakulima wetu kijikita katika kuzalisha vya kutosha ili kujiongezea kipato” Alisema Mhe.Mkirirkiti.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi kutambua kuwa Serkali ya awamuya tano imeweka msisitizo mkubwa kwenye kilimo ili kuongeza tija na kukifanya kilimo kuwa biashara.lengo ni kujihakikishia usalama wa chakula,upatikanaji wa malighafi za viwanda na kupata ziada ya kuuza nje na ili kufanikisha hayo sarikali itahakikisha pembejeo na zana bora za kilimo ikiwemo mbegu,mbolea,viatilifu/dawa na matrekta kwa uhakika na kwa gharama nafuu.
Katika kuhakikisha elimu ya kilimo bora inatolewa kwa wakulima wote wa Mkoa wa Manyara Mhe. Mkuu wa Mkoa aliwataka Wakurugenzi wote katika Halmashauri za Mkoa wa Manyara kuwaelekeza Maafisa ugani wawe karibu na wakulima na kutoa ushauri wa kitaalam wakati wa kilimo ili wakulima waweze kuongeza uzalishaji.
Akiongea wakati wa kumkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mrajisi Msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Manyara Bwana Venance Msafiri alisema kuwa madhumuni ya kikao kazi cha mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wakulima wadogo ili waweze kuzalisha kwa tija kwa kutumia zana bora katika uzalishaji.
Kwa upande wa wakulima walionesha kufurahishwa na mafunzo hayo kwani yameweza kuwakutanisha wakulima wadogo na wakubwa Pamoja na kujadili changamoto mbalimbali na kuona namna ya kuzitatua ili mkulima aweze kunufaika na kilimo kwa kutumia zana bora.
“Yaani mafunzo haya yatatusaidia sana kuongeza uzalishaji, na pia nawashauri waandaji wapanue wigo wa kutoa mafunzo mkoa mzima kwani wakulima tukikutana tunaweza kubadilishana uzoefu na kuwa na kilimo chenye tija” Alisama Bi.Stelleh Hombo Mkulima kutoka Mbulu.
Mafunzo hayo ya uhamasishaji wa matumizi bora ya zana za kilimo kwa wakulima wadogo na wakubwa kutoka wilaya ya Mbulu na Babati yameandaliwa na Ofisi ya Mrajisi Msaidizi wa vyama vya Ushirika Mkoa wa Manyara kwa kushirikiana na Kampuni ya Agri Crop Mechinization na Loan Agro Tanzania
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.