Serikali imepanga kuhesabu kwa mara moja watu wote watakaolala nchini kwenye usiku wa kuamkia siku ya sensa Agosti 23 mwaka huu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Mwigulu Lameck Nchemba ameyasema hayo mji mdogo wa Katesh Wilayani Hanang' Mkoani Manyara kwenye maadhimisho ya kitaifa ya siku ya idadi ya watu duniani.Waziri Nchemba amemwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ambaye ndiye alitarajiwa kuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa Mkoani Manyara.
Amesema serikali imejipanga na maandalizi yote yamekamilika ili kuhakikisha watu wote nchini watakaolala usiku wa kuamkia siku ya sensa wanahesabiwa kwa mara moja.Amesema mtu ambaye hatashiriki kuhesabiwa kwenye shughuli hiyo itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu atakuwa anarudisha nyuma jitihada za serikali kupata idadi kamili ya watu."Serikali ina mpango wa kuandaa dira ya Taifa ya miaka 25 hivyo sensa ni nyenzo ya maendeleo ya kufahamu idadi ya watu wake hivyo watanzania washiriki kwa pamoja," amesema Dkt Nchemba.Hata hivyo, ametoa rai kwa viongozi wa serikali kuhakikisha sensa ya mwaka huu inakuwa mfano na watu wote kushiriki ili kusaidia Taifa kupanga mipango ya maendeleo.
Mwakilishi mkazi wa shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani na makazi (UNFPA) Mark Bryan Schreiner amesema wakati Dunia inajiandaa kuwa na idadi ya watu bilioni 8 mwezi Novemba mwaka huu, watanzania nao wanapaswa kushiriki sensa itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu. Amesema asilimia 63 ya wananchi wa Tanzania ni vijana wenye umri wa chini ya miaka 25 hivyo watashirikiana na serikali kuwekeza kwa vijana hasa kwenye suala la afya."Pia tutashirikiana na serikali kwenye sensa ya mwaka huu, hivyo jamii ishiriki kikamilifu kuhesabiwa ili kufahamu idadi ya watu, wakiwemo wanawake, wanaume, wazee, vijana, watoto na makundi maalumu," amesema.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Laurence Mfuru amesema maadhimisho hayo yamefanyika Manyara kutokana na mwitikio wa viongozi na jamii ya eneo hilo.
Mfuru amesema mkoa wa Manyara una mwitikio mkubwa wa ufuatiliaji wa idadi ya watu, maendeleo ya sekta ya elimu, afya, maji, kupambana na ukatili wa kijinsia, hivyo ikapitishwa maadhimisho haya kufanyika Manyara.
Maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu ya 'Dunia ya watu bilioni 8 kuhimili wakati ujao ni fursa ya haki kwa wote, shiriki sensa kuhesabiwa kwa maendeleo endelevu'.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.