Wataalam wa Wizara ya Kilimo wametoa mafunzo ya kukabiliana na namna ya kuwatambua Nzige wa Jangwani ambao wamekuwa wakishambulia mimea katika nchi za Kenya, Uganda na Ukanda wa Kaskazini mashariki mwa bara la Afrika na janga la Nzige kwa Maafisa Kilimo na Maafisa Maendeleo ya Jamii Mkoani Manyara.
Bw. Juma Mwinyimkuu kutoka Kitengo cha Afya ya Mimea Kanda ya Kaskazini aliwaeleza washiriki kuwa Nzige ni wadudu hatari endapo watatua kwa makundi makubwa kwenye eneo moja kwa kuwa kila nzige moja ana uwezo wa kula mimea kiwango cha uzito wake kwa siku na ambayo ni sawa na gramu 20, hivyo kundi la Nzige laki tano wana uwezo wa kula Tani moja kwa siku. Alieleza kuwa Nzige hutembea katika makundi yenye wastani wa nzige milioni 10 hadi milioni 50 au Zaidi hivyo wanapotua katika eneo lenye mimea, mazao au misitu husabisha uharibifu mkubwa.
“Kila Nzige jike ana uwezo wa kutagaa mayai Zaidi ya 200 ndani ya kipindi cha wiki moja panapokuwa na mazingira ya unyevu,hivyo tahadhari inayotolewa ni kuwabini nzige hata wakiwa wachache ili kudhibiti uzalianaji wao kabla hawajawa kundi kubwa” Alisema Mtaalam huyo.
Kwa upande wa Mtaalam wa TPRI kitengo cha Unyunyiziaji wa Viuatilifu Bw. Justin Ringo aliwaeleza washiriki kuwa sumu inayotumika kuwadhibiti ni aina Fentrothion 96% ambayo iko chini ya Kundi la viuatilifu aina ya Organophosphate. Alisema kiuatilifu hicho kinasimamiwa na Wizara ya Kilimo na haiuzwi kwenye maduka ya Pembejeo. Aliwashauri wataalam hao kuhakikisha wanatoa elimu juu ya matumizi ya kiuatilifu hicho (Fentrothion 96%) na kuwaelimisha watumiaji kuchukua tahadhari kwa kuvaa mavazi maalum (overali+cloves, miwani maalum ya kulinda macho na viatu ili wakati wa kupulizia wadudu kwenye shamba mtu asiguswe na sumu kwenye ngozi ya mwili kwa kuwa sumu ikiingia kwenye mishipa ya damu inaleta madhara.
Alielezea upigaji wa sumu hiyo kwa njia mbili; njia ya kwanza ni kutumia aina tofauti ya mabomba maalum yanayobebwa mgongoni lakini aina ya pili ni kwa mashamba makubwa ambapo ndege maalum inatumika kupuliza kiuatilifu kutoka angani,lakini lazima kusiwe na watu au wanyama ambao wanaweza kudhuriwa na kiuatilifu hicho.
Wito ulitolewa kwa wataalam walioshiriki mafunzo hayo kwenda kusambaza ujumbe huo wa kuwatambua nzige wa jangwani na kutoa taarifa kutoka kwenye Vijiji, Kata kwenda Halmashauri, Mkoa na hatimaye Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kuchukua hatua za haraka za kusambaza viuatilifu na vifaa vya kupigia viuatilifu.
Mafunzo hayo yametolewa baada ya kutokea sintofahamu ya uvamizi wa Nzige nchini Tanzania hasa Mkoa wa Kilimanjaro.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.