Jopo la Wataalam kutoka Idara Mbali Mbali za Serikali wakiongozwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Wizara ya Afya, wanakusudia kuboresha Mitaala ya Vyuo vya elimu ya Afya huku nguvu kubwa ikielekezwa katika matumizi sahihi ya takwimu zipatikanazo kutoka katika vituo vya kutolea huduma za afya na matumizi yake.
Wadau hao waliokutana kwa siku moja mjini Morogoro, walisema kwa muda mrefu takwimu nyingi zinazopatikana kutoka katika vituo vya kutolea huduma zimekuwa zikukusanywa kwa mazoea na hivyo kubaki bila kutumika katika ngazi mbali mbali za maamuzi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa TEHAMA OR-TAMISEMI, Afisa TEHAMA, Melkiory Baltazari alisema, taaluma bora ni ile inayotafsiri maendeleo ya watu kwa vitendo na maendeleo hayo kuisaidia jamii.
“Tunazalisha data nyingi sana, lakini kiwango cha matumizi ya data hizo hakikidhi viwango tunavyo hitaji hususa ni katika ngazi za maamuzi alisema Baltazary na kuongeza kuwa, ukimfunza mtu, halafu taaluma yake hiyo ikatumika vizuri kwa kile kilicho kusudiwa utaona thamani ya elimu husika”.
Naye Mtaalam kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Issa Mbaga, alisema, umefika wakati suala la data likaingizwa katika mitaala ya vyuo vya wataalam wa Afya ili kuwajengea utamaduni wakuthamini takwimu pindi wawapo katika utekelezaji wa majuku yao ya kila siku.
Akizungumza wakati wa kutoa salaam za mradi wa PATH Tanzania, Mkurugenzi wa mradi wa Data Use Partnership Bi. Jackie Patrick, alisema anaipongeza Serikali kwa kuamua kuboresha suala la mifumo na matumizi ya takwimu kwa mapana yake kama yalivyoainishwa kwenya “Tanzania Digital Health Investments Roadmap 2017-2013”
“Sisi tunaipongeza sana Serikali ya awamu ya tano kwa namna inavyo weka msisitizo katika matumizi ya takwimu hususani zile tunazo zipata kutoka katika vituo vya kutolea huduma. Pia naipongeza serikali kwa kuamua kutumia ubunifu wa hali ya juu kujengea uwezo wa wahudumu wa afya kwa kuanzisha “Data Use Capacity Building Consortium” kupitia mradi wake wa Data Use Partnership ulioko chini ya wizara ya afya na Ofisi ya Rais – TAMISEMI. Alisema Bi. Jackie na kuongeza kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi chache Afrika kama sio pekee inayotumia ubunifu huu wa hali ya juu wa kutumia muungano “consortium” wa taasisi za kitafiti na taasisi za mafunzo za ndani ya nchi kujenga uwezo wa wahudumu wa afya kwenye matumizi ya takwimu. Huu ni ubunifu wa gharama nafuu na wa kudumu katika sekta ya afya” alihitimisha
Kando ya mafunzo hayo yakuwajengeana uwezo wataalam hao, Mkuu wa Chuo Uuguzi Ifakara, Prof. Florah Kessi, aliwaambia waandishi wa habari kwamba, lengo la Mafunzo hayo ni kuondokana na kufanya kazi kwa mazoea.
“Katika Mpango wa sasa, tunataka watoa huduma wanao ingia vyuoni na wale waliomaliza vyuo lazima sehemu ya mitaala yao, soma la ‘data use’ lipewe kipaumbele, maana walio wengi wanakusanya data lakini hawazitumi. ” alisema Prof. Kessy na kuongeza kuwa, mara kwa mara nimekuwa nikimsikiliza Mhe. Rais kwenye hutuba zake, kubwa analolifanya nikuongea kwa kutumia takwimu, lakini halikadhalika Mawaziri, Wabunge na viongozi wengine pia hawajaacha kutumia takwimu katika hotuba zao”.
Kwa upande wao washiriki wa semina hiyo, walisema wakati wa maboresho ya mitaala hiyo upo umuhimu wa kuwahusisha wataalam wa afya waliopo kazini ambao wana uzoefu lakini pia kutambua matumizi ya data walizo nazo.
“Tunapo andaa mitaala hii kwaajili kuiboresha mitaala yetu, tusiache kuwahusisha wakusanyaji, lakini pia watumiaji wa siku kwa siku ili kujiridhisha kwenye uhalisia wa data.” Alinikuliwa Faraja Makafu kutoka NACTE.
Akifunga Semina hiyo ya siku moja ya kujadili matokeo yaliyopatikana baada ya mchakato huo wakujadili kozi za muda mfupi na zile za muda mrefu kwa watumishi waliopo makazini na wale wanaojiunga na vyuo Mkurugenzi msaidizi wa huduma za afya Dkt. Anna Nswira kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, alisema katika hali ya sasa, mtaalam wa afya ndio Mchumi, Mwalimu, Mhandisi na ndio mwanasheria na taaluma zingine, hivyo wakati nchi inahubiri suala la uchumi wa viwanda hatutafikia huko kama wananchi watakuwa hawana afya njema.
Kukamilika kwa mtaala huo na kuanza kutumika katika vyuo vya kati na vyuo vikuu itasaidia kuimarisha matumizi ya data katika ngazi mbali mbali za maamuzi hususan wakati wa kupanga.
Anaandika Na: Atley Kuni- TAMISEMI
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.