Watu milioni 7.6 kila mwaka duniani hupoteza maisha kutokana na magonjwa ya Kisukari na Shinikizo la damu huku milioni 92 wakiathiriwa na Magonjwa hayo.
Hayo yamesemwa na Daktari wa Upasuaji kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara Dr.Ezekiel Morris Lukenza wakati akitoa mafunzo kwa Magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza kwa watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu kanda ya Kati (TFS) yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Dr. Lukenza amesema magonjwa hayo yanashambulia jamii na kuongeza gharama ya maisha ambapo ugonjwa wa Shinikizo la damu ndio unaongoza kupoteza nguvu kazi ya taifa.
Aidha Dr.Lukeza amesema ili jamii iweze kuepuka maradhi ya Moyo, kisukari na Ukimwi lazima kupima afya mara kwa mara kuuweka mwili vizuri kwa kufanya mazoezi na kuzingatia matumizi ya dawa pindi unapogundulika.
Pia amewataka watanzania kubadilisha mitindo ya maisha wanayoishi kwani ndio chanzo kikubwa cha kupata magonjwa haya yanayopoteza maisha ya wengi.
Naye Meneja Msaidizi wa Wakala wa Huduma za Misitu kanda ya kati Dodoma (TFS) Haji Khatibu, amesema katika mipango na bajeti wameweka shughuli za Mafunzo yanayohusu Magonjwa yasiyoambukiza na yanayoambukiza kama vile ukimwi na Shinikizo la Damu kwa watumishi wake ili wafahamu namna ya kujilinda na kuchukua hatua ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Amesema ni mpango wao wa kila mwaka kutoa Mafunzo ya aina hiyo kwa watumishi wa wakala wa Misitu ili kuimarisha utendaji wa kazi na kuwakumbusha kuwa Magonjwa hayo ni hatari kwa afya zao ambapo wanawatumia wataalamu wa afya katika mafunzo hayo.
Sambamba na hayo Wataalamu hao wa Misitu kutoka kanda ya kati inayohusisha mikoa ya Manyara,Arusha,Dodoma na Singida walipima na kuchangia benki ya damu.
Amesema wengine wanaweza kuona wanatumia rasilimali fedha lakini wao wanaamini Kinga ni bora kuliko Tiba hivyo wataendelea na utaratibu huo.
Aidha Haji amewataka watumishi hao wazingatie yote waliyofundishwa kwa kuyatilia mkazo kwa vitendo zaidi.
Akiyafunga mafunzo hayo ya siku mbili yaliyolenga kutoa elimu ya Rushwa na Afya,Katibu tawala wa mkoa wa Manyara Missaile Raymond Musa amewataka watumie fursa hiyo kama chachu ya kuepuka vitendo vya rushwa vinavyosababisha mazao ya misitu kupitishwa kimagendo.
Amesema mazao ya misitu kama zilivyo rasilimali nyingine za taifa ni muhimu katika kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja pamoja na kuongeza ajira.
Ameushukuru na kuupongeza uongozi wa Wakala wa huduma za Misitu kanda ya kati kwa kuuchagua mkoa wa Manyara kwa mara ya pili mfululizo kufanyia mafunzo ya magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza na kwa sababu imechangia kwenye pato la mkoa kwa huduma mbalimbali walizozipata na kuongeza mahusiano mazuri ya kitaasisi.
Imeandikwa Na: John Walter
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.