Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli leo amemuapisha Mh Joseph Joseph Mkirikiti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara pamoja na viongozi wengine mbalimbali walioteuliwa jana na Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mkirikiti amechukua nafasi ya Mheshimiwa Alexander Pastory Mnyeti ,kabla ya uteuzi huo Mheshimiwa Mkirikiti alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara.
Baada ya kukamilika kwa zoezi la uapishaji Viongozi wachache wamepewa nafasi ya kutoa salaam. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Chalamila amepewa nafasi ya kutoa salam kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa ambapo amemshukuru Rais Magufuli kutokana na fedha mbalimbali zilizotolewa ili kutekeleza miradi ya maendeleo katika mkoa wa Mbeya na kuahidi kuendelelea kutimiza majukumu yake ya ukuu wa Mkoa katika jiji hilo.
Katika kueleza hili Mh. Albert Chalamira anasema "Katika jiji la Mbeya wachache wamesema hakuna maendeleo yanachotekelezwa lakini hivi karibuni tumepokea zaidi ya bilioni 3.6 kwa ajili ya miundombinu ya Elimu. Hili ni moja ya mambo yaliyonifanya nibaki jiji la Mbeya bila kwenda kugombea"
Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kutoa salamu kwa sasa amekaribishwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi General Salvatory Mabeyo ambaye anatoa salamu kwa niaba ya Vyombo vya Ulinzi na usalama. General Mabeyo ambapo ameshukuru kwa kupewa nafasi hiyo pamoja na kuwapongeza viongozi wote walioteuliwa na kuwasisitiza kwenda kutimiza majukumu yao.
General Mabeyo amesema "Kwa niaba ya wenzangu nawapongeza walioapishwa kwenda kushika madaraka yao. Lengo kubwa ni kwenda kuwatumikia wananchi lakini kubwa ni kujitafakari na kujitambua kuwa tunapotumikia nafasi zetu tujue dhamana hiyo ni kwa ajili ya maendelo ya Taifa na Wananchi"
Waziri wa Tamisemi Mh. Seleman Jafo amekaribishwa kwa ajili ya kutoa salamu. Aidha, Mh. Jafo amewapongeza Viongozi wote walioteuliwa pamoja na kuwasisitiza wote kwenda kutimiza majukumu yao.
Katika hili Mh. Seleman Jafo amesema "Viongozi mlioapishwa tukamsaidie Rais, tusiende kutafuta umaarufu bali umaarufu uwafuate ninyi. Wanaotafuta umaarufu mara nyingi mwisho wao sio mzuri sana. Nendeni mkahakikishe zile fedha ambazo Rais amezielekeza huko mnazisimamia"
Sambamba na hilo, Jafo amesema Tangu Rais ameingia, ‘trend’ ya udhibiti wa fedha za mamlaka za Serikali za Mitaa umeongezeka kwa umakini mkubwa. Nendeni mkatimize majukumu yenu. Huwa haipendezi unatoka hapa unafika ‘site’ jukumu alilotakiwa kufanya Mkuu wa Wilaya hajafanya. Tembeleeni miradi"
Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan amewapongeza viongozi wote walioteuliwa na kuapishwa katika nafasi mbalimbali. Pia, Mh. Samia amewasisitiza viongozi hao kwenda kutekeleza majukumu yao.
Zaidi ya hayo, Mama Samia Suluhu amewaonya viongozi na kuwasisitiza viongozi kuridhika na madaraka wanayopewa. katika hili Makamu wa Rais amesema Imempendeza Rais kuwapa madaraka akiamini mtakwenda kuwatumikia watu. Mwanadamu unapoishi unatakiwa kutosheka. Utawala wetu sasa hivi sio utawala wa kuhaha na madaraka. Kuwatumikia watu sio kuwaongoza, nendeni someni na angalia wapi pa kurekebisha
HOTUBA YA RAIS MAGUFULI
Rais Magufuli amewapongeza viongozi wote walioapishwa siku ya leo pamoja na kuwasisitiza kwenda kuwatumikia Wananchi wote kwa bidii. Zaidi ya hayo Rais Magufuli amewasisitiza Viongozi walioteuliwa kuridhika wanapopewa madaraka mbalimbali.
Rais Magufuli amesema "Mtambue kwamba hizi nafasi mmezipata kwasababu Mwenyezi Mungu alitaka. Mkawatumikie Wananchi hasa Wananchi masikini. Dkt. Luhende umekuwa Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar. Kanali Songea tumekupeleka Kiteto migogoro ipo mingi, tumekupeleka ukaishughulikie.
Katika hili Rais Magufuli amesema kuwa "Kwenye hizi kazi kuridhika ni kitu kikubwa. Yule kijana pale anaitwa Selemani ana PHD lakini mshahara ni laki 5. Aliridhika na mshahara wake. Ilipojitokeza fursa ndiyo tukamteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa. Mmefanikiwa kuipata fursa, hivyo mkafanye kazi". Aidha, katika hili Rais Magufuli ametoa mifano ya viongozi mbalimbali walioteuliwa na namna walivyovumilia katika majukumu mbalimbali.
Rais Magufuli amesema "Viongozi vijana imekuwa ngumu kuridhika hasa waliozaliwa miaka ya 1982. Nilikuwa napewa taarifa na Makamu wa Rais kuwa waliojitokeza kugombea kupitia CCM mpaka sasa ni zaidi ya 8,000 na Dar es Salaam ndiyo inaongoza ambapo hadi leo alfajiri wapo 829" .
Aidha, Rais Magufuli amesisitiza kuwa hajamtuma kiongozi yoyote kwenda kugombea nafasi yoyote. Hivyo, viongozi waliochukua fomu ndani ya chama hicho wapimwe inavyostahili.
Katika jambo hili Rais Magufuli amesema "Nataka kuwathibitishia wananchi na wanaCCM hakuna mtu yeyote aliyetumwa na mimi, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mzee Mangula wala Katibu Mkuu Dkt. Bashiru. Kama wapo watu kule wanaozungumza huko wametumwa na Rais ni waongo. Wapimeni wagombea itakavyowafaa" Siwezi kutuma mtu nyuma ya mgongo".
"Kama ningekuwa na uwezo wa kukutuma wala nisingehangaika, ningesubiri kwenye viti vyangu 10 nikakuteua. Mtu asijekusema ametumwa na IGP au na CDF, wangetaka wangekuteua kuwa hata Kanali. Nendeni mkatumwe na wananchi huko, kila mahali kuna tatizo lake"
zaidi ya hayo rais Magufuli amesisitiza viongozi hao kwenda kuwatumikia wananchi. Mathalani, akimuongelea Mkurugenzi wa TIC Rais Magufuli amesema amemtaka kiongozi huyo kuhakikisha anatafuta Wawekezaji wengi.
Katika jambo hili Rais Magufuli amesema "Kumekuwa na tabia ya kuwazungusha wawekezaji. Mwekezaji amekuja na pesa lakini wewe mara njoo huku mara njoo kesho. Msiwazungushe wawekezaji maana wakiwekeza tutatengeneza ajira. Kuna mwekezaji anataka kujenga kiwanda cha vifaa vya umeme ila nasikia amezungushwa"
Zaidi ya haya Rais Magufuli amewasisitiza kuwa "Kila mmoja katika eneo lake akafanye ambavyo anaona inafaa sio kwamba tumekuwa tukifanya hivi. Tuongeze ‘speed’ na tunataka twende ‘speed’ kubwa zaidi ‘We used’ inakuwa ‘past tense’ kwenye kiingereza, ‘We do this’ hicho ndicho ninachotaka kila mtu akashughulikie"
Mwisho, Rais amewashukuru na kuwatakia mafanikio mema wote walioteuliwa pamoja na kupiga nao picha za kumbukumbu.
Viongozi Wateule walioapishwa Leo ni:
1. Bw. Aboubakar Kunenge- Kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
2. Bw. Joseph Joseph Mkirikiti - Kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara
3. Bw.Paulo Mshimo Makanza - Kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam
4. Bw. Gabriel Pascal Malata- Kuwa Wakili Mkuu wa Serikali
5. Dkt. Boniface Luhende-Kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali
6. Dkt. Maduhu Isaac Kazi - Kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)
Pia Mhe. Rais alishuhudia Uapisho wa Wakuu wa Wilaya za Hanang, Kiteto, Kongwa, Chunya na Moshi
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.