Na Nyeneu, P. R - Mjini Babati
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga amefungua Warsha na Mkutano mkuu wa mwaka 2024 wa Chama cha Wakutubi Tanzania chenye lengo la kujadili Mabadiliko kwa ajili ya Mazingira Endelevu ya Kidijitali katika Ukutubi na Sayansi kilichofanyika Mjini Babati Februari 26, 2024.
Mhe. Mkuu wa Mkoa akijibu hoja iliyotolewa kwenye risala ya chama hicho kuhusu mkoa wa Manyara kukosa maktaba, ameahidi kuwa Ofisi ya mkuu wa Wilaya wameahidi kutoa eneo kwaajili ya kuanza ujenzi mara moja wa maktaba ya mkoa. Aidha sendiga amewashauri wakutubi nchini kuwa sehemu ya kusoma vitabu badala ya kuwa watunzaji pekee katika maeneo wanakofanya kazi hiyo ya ukutubi.
Vilevile Mkuu wa Mkoa amekipongeza Chama cha Wakutubi Tanzania kwa uamuzi wao wa kuchagua Mkoa wa Manyara, na hususan Mji wa Babati kuja kufanyia Warsha na Mkutano Mkuu wa mwaka kwa mara ya kwanza tangu Chama kilipoasisiwa mwaka 1973. “Naamini uchaguzi ulitokana na sio tu urahisi wa kufika hapa Babati kutokea kona zote za Jamhuri yetu, bali pia uwingi na ubora wa vivutio vya utalii vya kiwango cha kimataifa, Hongereni sana”. Alisema Mkuu wa Mkoa.
RC Sendiga amewashauri Chama cha Wakutubi nchini kuongeza ubunifu katika kuendana na kasi ya utandawazi ili kuweza kuhamasisha jamii kujitokeza kusoma vitabu. Mkuu wa Mkoa ameongeza na amesema ni lazima Chama hicho sasa kifikirie mbali zaidi katika kukuza na kubadilisha sekta hiyo ya usomaji wa vitabu ili kuendana na ulimwengu wa kidijitali.
Akisoma risala yao kwa mgeni rasmi Ndg LEONTIN NKEBUKWA Mwenyekiti wa TLA ameiomba serikali kuingilia kati tabia ya waajiri wa baadhi ya taasisi kutowapa haki wakutibu wao kujiunga na Chama hicho hali inayopelekea kukosa fursa ya kueleza kero mbalimbali zinazowakabili kupitia Chama hicho.
Pamoja na hilo ndg Nkebukwa ameomba uwekezaji ufanyike kwenye sekta hiyo katika uwekezaji wa miundombinu ya kidijitali kuendana na kasi ya mabadiliko ya dunia ya sasa ambapo ametaja baadhi ya mahitaji muhimu kuwa ni pamoja na kompyuta na kamera.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.