Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Joseph Joseph Mkirikiti amewataka wananchi wa Mkoa huo pamoja na mikoa ya jirani kujiandaa na mashindano ya ngumi Kitaifa yanayotarajiwa kuanza kufanyika Septemba 6, 2020 Mkoani humo.
Mheshimiwa Mkirikirti ameyasema hayo jana Agosti 24 alipokuwa akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Motel Papaa Mjini Babati.
“Ngugu wananchi wa Mkoa wa Manyara kuanzia mwezi wa tisa tunatarajia kuwa na mashindano yabondia Kitaifa yatakayofanyika hapa makao makuu ya Mkoa kwa kukutanisha mabondia kutoka mikoa yote ya Tanzania bara, hivyo nawataka mjiandae kupokea ugeni huo na pia muanze kufanya maandalizi mbalimbali kwani ugeni huo utakuwa na fursa mbalimbali katika Mkoa wetu” Alisema Mhe.Mkirikiti.
Katika kujiandaa na mashindano hayo Timu ya Bondia ya Mkoa wa Manyara tayari imeshapatikana kwa kufanya mchujo wa mabondia kutoka wilaya zote tano za Mkoa na ipo kambini tangu Agosti 5,2020 ili kuhakikisha wanachukua ubingwa wa Taifa.
Fursa mbalimbali kama za usafirishaji,Huduma za chakula, malazi,huduma za simu na nyingine nyingi zinaweza kupatikana kutokana na mahindano hayo na hivyo kuwafanya wakazi wa Manyara kujiongezea kipato chao na kwa Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Manyara amewataka wananchi kufanya kazi kwa bidi na kuacha kujihusisha na vitendo vya kihalifu kama uvutaji bangi,utumiaji wa madawa ya kulevya, vitendo vya ubakaji na tabia za wizi.
“Pamoja na Mji wetu wa Babati kuachangamka na kuonesha sura ya kuwa Makao Makuu ya Mkoa bado kuna watu wachache wanatuletea sifa mbaya katika Mkoa wetu kwa vitendo vya ajabu ajabu,hivyo nawataka wote wenye vitendo hivyo kuacha mara moja la sivyo hatua kali za kisheria zitafuata kwa kuwafuatilia wote na kuwakamata” Alisisitiza Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara ambaye yupo katika ziara ya kujitambulisha kwa wananchi tangu ateuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli pia alisikiliza kero mbalimbali kwa wananchi wa Mji wa Mji Babati na kuzitafutia ufumbuzi kwa kuwataka wataalamu wa Halmashauri zote za Mkoa huo kujenga utaratibu wa kutatua kero za wananchi mapema ili kuondoa manung’uniko kwa wananchi.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.