Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ustawi wa Jamii Ofisi ya Rais Tamisemi, Rasheed Maftah ameitaka mifumo inayokusanya taarifa za ustawi wa jamii katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuungana na kuwa mfumo mmoja unaotoa taaarifa zote zinazohitajika katika kuhudumia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Maftah ameyasema hayo wakati wa kikao maalum cha kuwapitisha wataalamu na wadau kwenye mfumo wa Ustawi wa Jamii wa taarifa za watoto walio katika mazingira hatarishi (MVC-MIS) unaowezeshwa na Taasisi ya MEASURE Evaluation; Kikao hicho kilifanyika kwenye ukumbi wa Reform OR-TAMISEMI mwishoni mwa juma lililopita.
Kupitia kikao hicho wataalamu wa mifumo hiyo waliweza kuwapitisha wadau kwenye mfumo unaoenda sanjari na MVC-MIS ambao ni USSD unaowezeshwa na Taasisi ya pact kizazi kipya.
Maftah alisema ni wakati sasa waataalamu wetu kukutana pamoja na kuona namna gani mifumo hiyo ambayo inakusanya taarifa za ustawi wa jamii kuungana na kuwa na mfumo mmoja ambao utafanya kazi zote zinafanywa na mifumo hiyo kwa sasa.
Aliongeza kuwa kazi hiyo ni lazima ifanywe na wataalamu wa mifumo toka Ofisi ya Rais –TAMISEMI pamoja na Wizara ya Afya wakishirikiana na wale waliotenegneza mifumo hiyo hapo awali kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Measure Evaluation pamoja na Path Kizazi Kipya.
“Ni wakati sasa wa wataalamu wetu kujengewa uwezo na kuifahamu mifumo hii kwa undani na kushiriki katika kuiunganisha ili hapo baadae miradi itakapomaliza muda wake na kuikabidhi mifumo hiyo kwa Serikali tuwe na wataalamu watakaoweza kuindeleza na kuisimamia wadau wetu wanavyofanya sasa” alisema Maftaha.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma toka Ofisi ya Rais TAMISEMI Angelista Kihaga akichangia wakati wa kikao hicho alisema hata kama mifumo hii inawezeshwa na wafadhili lazima waangalie uwezekano wa kuwajengea uwezo zaidi watumishi wa Serikali ambao wataendelea kuihudumia mifumo baada ya mradi kwisha kuliko kuajiri watumishi wa muda au kuwajengea uwezo wataalamu wa kujitolea “Volunteers” ambao huondoka mara tu mradi unapomaliza muda wake.
“Sisi kama Serikali lazima tuangalie namna ambavyo mifumo hii inakua endelevu na sio siku wadau wakitukabidhi mifumo baasi ndio inakua mwisho wa matumizi ya mifumo hiyo sio sawa; Imefika wakati ambapo wataalamu wanatakiwa kufahamu kila kitu katika mifumo hii ili waweze kuiendeleza hapo baadae” alisema Kihaga.
Awali akiwapitisha wataalam katika Mfumo wa MVC-MIS Bi. Immaculate Ayebazibwe Kutoka MEASURE Evaluation alisema kuwa mfumo wa MVC-MIS unawezesha ukusanyaji wa takwimu sahihi zinazofanikisha upatikanaji wa taarifa za utawi wa jamii, na pia unafanya uchambuzi wa kina wa tawkimu hizo.
Naye Mtaalamu kutoka Pact Kizazi Kipya Bw. Tumaini Mbwambo ambao anasimamia mfumo wa USSD wa kukusanya taarifa za ustawi wa jamii alisema kuwa mfumo wao unakusanya zaidi taarifa binafsi tofauti na ule wa MVC-MIS unaokusanya taarifa kwa makundi.
Wakati huo huo mtaalamu kutoka TASAF Bw. Sesil Latemba alipata furasa ya kuwapitisha wajumbe kwenye mfumo unaotumiwa na TASAF katika kukusanya taarifa za Kaya Masikini kuomba kikao hicho kuona uwezekano wa kuunganisha mfumo huo na ule wa usatwi wa jamii.
Mfumo huu wa kielektroniki wa ukusanyaji wa taarifa za watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi wa MVC-MIS unatumika katika halmashauri 67 Nchini na hivi karibuni utafikishwa kwenye halmashauri 106.
Mfumo huu umekuja kuhuisha ile njia ya awali ya kutumia regista Namba 1 ambayo hutumika kuorodhesha majina ya watoto wote wanaoishi kwenye mazingira hatarishi katika kijiji au mtaa husika ambao kwa kila mdau anayehitaji kusaidia watoto hao inamlazimu kupitia regista hiyo kuona majina ya watoto wanaohitaji msaada wa kiustawi.
Na: TAMISEMI
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.