Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe.Joseph Mkirikiti ameipongeza shule ya msingi Lalakir iliyopo wilayani Kiteto kwa kushika nafasi ya kwanza Mkoa wa Manyara katika matokeo ya Mitihani ya darasa la saba mwaka 2020.
Mhe. Mkirikiti ametoa pongezi hizo jana alipoongea na walimu na wanafunzi wa shule hiyo alipotembelea shuleni hapo kukagua miradi ya Education Performance for Results (EP4R) na ujenzi wa miundombinu ya vyoo bora na miundombinu ya maji kupitia program ya usafi wa mazingira na usambazaji wa maji vijijini (SRWSS).
“Napenda kuwapongeza walimu,wanafunzi,wazazi na wadau wote was hule hii kwa ushirikiano wenu wa kuhakikisha Watoto wetu wanapata elimu bora, na kwa kweli watoto wa wafugaji wakiwekewa mazingira mazuri ya kusoma wanasoma sana!!” Alisema Mhe.Mkirirkiti.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa pia amewapongeza walimu katika shule hiyo kwa kuonesha upendo miongoni mwao na kwa wanafunzi kitu kinachofanya kuongezeka kwa ufaulu shuleni hapo.
Akisoma risala mbele ya Mkuu wa Mkoa, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo alisema kuwa shule hiyo imekuwa ikishika nafasi yay a kwanza Kimkoa na Kiwilaya kwa miaka mitano mfululizo na mwaka huu wamefanya mitihani wanafunzi 33 na kati ya hao wanafunzi 32 wamefaulu kwa daraja A na Mwanafunzi 1 tu amepata daraja B na shule imepata wastani wa alama 219.1212 ambayo ni daraja A na hivyo kuifanya kuwa shule ya kwanza katika Mkoa wa Manyara
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa mafanikio hay ani matokeo ya upendo na ushirikiano miongoni mwa walimu,wanafunzi, viongozi wa kamati, jamii na serikali kwa ujumla. Aidha walimu wanafanya kazi kwa bidi,ubunifu na kujituma mno kiasi kwamba wanafundisha usiku na siku za mwisho wa juma” Alisema Mwalimu Mkuu wa shule hiyo.
Mara baada ya taarifa hiyo kutoka kwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mkuu wa Mkoa alifurahishwa san ana jinsi walimu wa shule ya Lalakir wanavyoishi kwa upendo na wanafunzi na jinsi wanavyojitolea na pia alianzisha harambee kwa msafara mzima uliombatana nao kuwachangia wanafunzi na kufanikiwa kuchangisha shilingi laki mbili na elfu arobaini na mbuzi mmoja ili wanafunzi wabadishe chakula kwa siku hiyo Pamoja na kuwapatia wanafunzi wa shule hiyo zawadi ya mpira mmoja wa wavulana na kumtaka Mkurugenzi wa Wilaya ya Kiteto Bwana Tamim Kambona kuwaletea mipira ya pete kwa ajili ya wasichana.
Mkuu wa Mkoa wa Manayara Mhe.Joseph Mkirikiti akikabidhi zawadi ya Mpira kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Lalakir iliyopo Wilayani Kiteto.
Shule ya msingi Lalakir ni miongoni mwa shule zilizonufaika na ujenzi wa miundombinu ya vyoo bora na miundombinu ya maji kupitia Programu ya usafi wa mazingira na usambazaji wa maji vijijini (SRWSS) kwa kupatiwa jumla ya shilingi Milioni nane laki nane elfu kumi na saba na mia tano (8,817,500)
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.