Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Joseph Mkirikiti amefurahishwa na mradi wa maji wa Mayoka- Minjingu unaogharimu shilingi bilioni mbili unaojengwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) unaotarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi Februari 2021.
Mhe.Mkirikiti ameonesha furaha hizo jana baada yaye na kamati ya siasa Mkoa wa Manyara kutembelea mradi wa maji Mayoka-Minjingu unaosimamiwa na RUWASA na kuwakuta mafundi wanaojenga mradi huo wapo katika hatua za mwisho za kuunganisha bomba kilomita 13 kukatiza kati kati ya ziwa Manyara ili kukamilisha mradi huo.
Mara baada ya kufika katika chanzo cha ujenzi huo katika Kijiji cha Mayoka Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na Kamati ya Siasa walipata maelezo kutoka kwa Meneja wa RUWASA Mkoa wa Manyara Mhandisi Wolta Kirita ambaye alisema kuwa mradi huo mpaka sasa wameshalaza bomba kilomita 4 kutoka kwenye chanzo hadi Kijijini hapo na Kilomita 10 zimelazwa ziwa Manyara na fedha zinazotumika kukamilisha mradi huo zinatoka RUWASA Makao Makuu na mara baada ya kukamilika unatarajia kuhudumia wakazi zaidi ya 15000 katika vijiji vya Olasiti,Minjingu,Kakoi, Vilima Vitatu na Mayoka.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa mradi huu unasimamiwa na RUWASA wenyewe na mpaka utakapokamilika utatumia shilingi bilioni mbili na tunatarajia utamaliza kero ya upatikanaji wa maji katika kata ya Nkaiti na baadhi ya vijiji vya kata za Mwada na Magara” Aliongeza Mhandisi Wolta Kirita.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Manyara pia alimuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa mradi huo utamalizika Mwishoni mwa mwezi februari 2021 baada baada ya kushindwa kumalizika Disemba mwaka 2020 kutokana na changamoto ya mvua iliyosababisha ziwa kujaa.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Mradi huu ulitazamiwa kumalizika Disemba 2020 lakini kutokana na changamoto za mvua na kwa sasa tumeazima boti kutoka Halmashauri ya Mji Babati na Halmashauri ya Wilaya ya Babati ili kuhakikisha mradi unakamilika Februari 2021 na ili wananchi waanze kupata maji safi na salama” Alisisitiza Mhandisi Kirita.
Akielezea jinsi alivyofarija na jinsi RUWASA wanavyohakikisha mradi huo unakamilika Mheshimiwa Mkuu aliwapongeza RUWASA kwa kukamilisha miradi ya maji katika Mkoa wa Manyara hasa katika mradi huo wa Mayoka-Minjingu.
“Mimi na kamati ya siasa Mkoa tumefarijika sana kuona mradi huu umefikia asilimia 80 na Meneja wa RUWASA kutuhakikishia kumalizika ifikapo Februari 2021 na pia tumeona kabla mradi kwisha wananchi wa Kijiji cha Mayoka wanaendelea kupata huduma kupitia bomba kuu kabla kuunganishiwa katika vituo vya kuchotea maji” Alisema Mhe.Mkirikiti.
Wakielezea furaha yao wananchi wa Mayoka wamesema kuwa wameridhika na mradi huo kwani katika Kijiji chao watawekewa vituo 8 vya kuchotea maji na hivyo kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kufuata maji.
“Kiukweli sisi wana Kijiji tumefurahi sana kuletewa maji na Serikali yetu kwani zamani tulikuwa tunakunywa maji kutoka ziwani ambayo siyo salama lakini kwa sasa tumeshaanza kunywa maji safi na salama na baada ya RUWASA kutujengea hivyo vituo vya kuchotea maji na sehemu za kunyweshea mifugo yetu hali itakuwa nzuri sana!! Na tunaahidi kuutunza mradi huu ili usiharibiwe” Alisema Mama Isabela wa Kijiji cha Mayoka.
Pamoja na Mradi na Maji Mayoka- Minjingu Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa pia alitembelea miradi ya Maji katika Kijiji cha Endakiso na Mutuka Wilayani Babati.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.