Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mh. Alexander Mnyeti amefanya ziara ya siku nne kuanzia tarehe 23 hadi 26 katika Halmashauri ya Mji Babati kwa kuongea na watumishi wa Halmashauri,kukagua miradi ya maendeleo iliyomo katika Halmashauri hiyo na kufanya mikutano ya hadhara kwa kusikiliza kero zinazowakabili wananchi na kuzitatua.
Katika siku ya kwanza ya ziara hiyo Mh.Mkuu wa Mkoa aliongea na wafanyakazi wa Halmashauri ya Mji Babati alilipongeza Baraza la Madiwani kwa kufanya kazi vizuri pamoja na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo vilevile aliwapongeza wakuu wa shule zote za Mkoani Manyara zenye kidato cha tano na sita kwa kufaulisha kwa asilimia mkia katika mitihani ya Taifa kwani katika wanafunzi 1000 waliosajiliwa wanafunzi wote wamefaulu.Pia aliwataka wafanya kazi wa Halmashauri hiyo kuwatumikia wananchi vizuri ili kusiwe na malalamiko ya mara kwa mara hasa upande wa Idara ya Ardhi na Fedha.
Mkuu wa Mkoa pia aliitaka Halmashauri kuhakikisha inatoa asilimia tano kwa wanawake na asilimia tano kwa vijana katika kuwapa mikopo isiyo na riba.
Baada ya kiako hicho na wafanyakazi Mh.Mkuu wa Mkoa wa Manyara alitembelea mradi wa maji uliopo Kata ya Bonga, Kijiji cha Haraa na kuweka jiwe la msingi na kuwataka wananchi kuilinda miundombinu ya maji kwani miundombinu hiyo inawekwa kwa gharama kubwa sana, pia aliwahakikishia wananchi wa Kijiji hicho kuwa kabla ya mwaka 2020 vijiji vyote ndani ya Mkoa wa Manyara na vitakuwa na huduma ya maji chini ya Serikali ya awamu ya Rais John Pombe Magufuli.
Vilevile Mh.Mnyeti alitembelea Shule ya Msingi Gendi kujionea ujenze wa vyoo bora na ukarabati wa majengo katika shule hiyo, kiwanda cha Unga wa Sembe katika kuhakikisha Tanzania ya viwanda katika Kata ya Singe na kiwanda cha mafuta ya Alizeti kilichopo Kata ya Nangara.
Pia Mh.Mkuu wa Mkoa alitembelea Shule ya Sekondari ya Nakwa inayojengwa ili kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu wanafunzi kutoka Nakwa hadi Shule ya Sekondari Bagara,Shule hiyo inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2019.
Mh. Mnyeti alipata fursa ya kutembelea shule ya Msingi Qares na Zahanati ya Nakwa na kufurahishwa na jinsi ya wanakijiji kuweza kusimamia miradi ya maendeleo.
“Nimefurahishwa sana na wana Nakwa na miradi yenu!! Kwa miradi hii nawapa nafasi ya kuchagua mradi mwingine na mimi nitachangia asilimia 75 ya mradi huo mtakaouanzisha” Alisema Mkuu wa Mkoa.
Vilevile katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Manyara alitembelea kiwanda cha vinywaji vikali kilichopo Mtaa wa Bagara Ziwani,viwanda vya Mafuta ya Alizeti vilivyopo Kiongozi na Maisaka A,Shamba la Kahawa lililopo Kijiji cha Managhat,Barabara za lami zinazojengwa na Serikali mjini Babati,Viwanja vya Singu na Maisaka katani, Standi Mpya iliyopo Maisaka Katani na Eneo kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa michezo.
Pamoja na kutembelea miradi ya maendeleo Mh.Mkuu wa Mkoa wa Manyara alifanya mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali na kuitaka idara ya ardhi mjini Babati kutoa hati miliki kwa wote wenye viwanja Maisaka A Babati Mjini ndani ya siku tisini.
Agizo hilo amelitoa kwenye mkutano wa wananchi uliofanyika shule ya msingi Sinai kusikiliza malalamiko ya wakazi wa Maisaka.
Kwa mujibu wa Mnyeti,agizo hilo ni la Rais Magufuli baada ya kusoma na kutazama taarifa ya Habari baada ya nyumba zilizokuwa zimejengwa kiholela katika eneo la Maisaka A kuwekewa alama ya X iliyosababishwa na uzembe wa idara ya ardhi na mipango miji.
Mnyeti amesema kuwa hati hizo atakabidhi mwenyewe kwa wananchi tarehe 25 Oktoba mwaka huu na kuwataka wananchi wote ambao bado nyumba zao zina X wakazifute waishi kwa uhuru.
"Kwa Tanzania ukitaka kubomoa waliojenga Kiholela ni asilima 75% serikali imeona iwaache ambao tayari wameshajenga kwa sababu serikali kupitia idara ya Ardhi na Mipango miji ilishakosea kuwaachia watu hao kujenga bila kufuata utaratibu” alisema Mnyeti.
Hata hivyo ametoa onyo kwa wanaoendelea kujenga katika maeneo ambayo sio rasmi huku akitoa onyo kwa waliojenga kwenye milima.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara pia amesema hatakubali kuona maamuzi mabovu yanatolewa kwenye mkoa wake ikiwemo kufungia kiwanda bila sababu ya msingi.
Mnyeti ameyasema hayo mjini Babati baada ya kiwanda cha pombe cha Mati Super Brands Ltdkufungiwa bila sababu za msingi.
Alisema viongozi wa serikali wanapaswa kuwa wasaidizi kwa kuwaelewesha kitaalamu wawekezaji ili warekebishe mapungufu pindi yakiwepo na siyo kufungia viwanda.
Alisema hivi sasa serikali ipo kwenye mchakato wa ujenzi wa viwanda vipya hivyo wataalamu wanatakiwa kutumia elimu yao kuwaelimisha wawekezaji na siyo kuwakandamiza.
“Hizo mbwembwe kafanyie sehemu nyingine siyo Manyara, haiwezekani mtu eti anajiita mtaalamu wa serikali anafungia kiwanda sababu ya ukosefu wa komeo la mlango au kuwa na eneo dogo la kuhifadhi bidhaa,” alisema Mnyeti.
Mkurugenzi wa kiwanda cha Mati Super Brands Ltd, David Mlokozi alisema ili kuunga mkono kauli ya Tanzania ya viwanda wapo mbioni kuanzisha viwanda vingine mkoani Manyara.
Hivi karibuni Mlokozi alisema watamuomba mkuu huyo wa mkoa afungue kiwanda kingine cha vinjwaji vikali ili kukuza uchumi wa nchi na kutoa ajira kwa wananchi wa eneo hilo.
Pia aliwataka wananchi wa Kijiji cha Singu kuacha kuvamia maeneo na kutii sheria zilizowekwa katika kusuluhisha migogoro ya ardhi katika eneo lao.
(Kwa Video mbalimbali za ziara hiyo angalia sehemu ya Video na Picha mbalimbali angalia sehemu ya Maktaba ya Picha)
Imeandikwa na:Haji A. Msovu(Afisa Habari Mkoa wa Manyara)
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.