Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe.Joseph Mkirikiti amezitaka jamii kuwaheshimu wazee katika maeneo yao kwani wazee ni watu muhimu katika Taifa lolote.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo leo katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa alipokuwa anazindua Baraza la Wazee la Mkoa wa Manyara.
“Sisi vijana tusijisahau sana kuwatahamini wazee kwani lazima tukumbuke kuwa tusipowaheshimu wazee ipo siku siku na sisi tutakuja kuwa wazee kwa hiyo lazima tuwaheshimu wazee ili na sisi tuje kuheshimiwa tukiwa wazee” Alisisitiza Mhe.Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa mkoa amesema kuwa ni lazima kila Halmashauri ihakikishe inawatambua wazee wote ili wapewe huduma stahiki kulingana na uhitaji wao,kuhakikisha ifikapo Desemba 2020 wazee wote wawe wamepata vitambulisho vya matibabu bure na pia kuhakikisha katika Hospitali,Vituo vya Afya na Zahanati ndani ya Mkoa wa Manyara kunakuwa na madirisha ya Wazee ili kuwafanya wazee hao kupata huduma kwa haraka.
“Ndugu wajumbe wa baraza la wazee Mkoa wa Manyara napenda kuwahakikishia kutatua changamoto zote zinazowakabili wazee mkoani kwetu ikiwemo kuzipa elimu baadhi ya familia kwenye baadhi ya maeneo kuwatelekeza wazee kwani na sisi ni wazee watarajiwa” Alisema Mhe Mkirikiti.
Katika kuhakikisha wazee hawatengwi Mkoa wa Manyara umeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuhakikisha wazee wanakuwa na jukwaa lao la kusemea mambo muhimu yanayohusu maslahi yao,kushawishi mambo ya wazee kujadiliwa kuanzia ngazi ya kijiji hadi ngazi ya wilaya,kuhakikisha wazee wanakuwa na uwakilishi kama vile halmashauri ya kijiji,WDC,Baraza la Madiwani,DCC na RCC ilikuweza kushauri vyema mambo mbalimbali ya wazee na kuwahimiza wazee kuunda vikundi vidogovidogo vya ujasiriamali kwa ajili ya kuzalisha mali jambo ambalo litawasaidia kujipatia mahitaji yao madogomadogo ya kila siku.
Vilevile Mkuu wa Mkoa alisisitiza ndani ya baraza hilo kujiepusha na ubaguzi wa aina yoyote.
“Ndugu wajumbe naapenda ikumbukwe kuwa Mabaraza ya Wazee ni huru,si yakiitikadi,kidini au ukabila na kila mtummwenye umri wa miaka 60 na kuendelea ana haki ya kuwa mjumbe wa baraza la wazee” Alisisitiza Mhe. Mkuu Mkoa.
Akizungumzia juu ya uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi kuwapa kipaumbele wazee na makundi maalumu yote ikiwemo wagonjwa, wenye watoto ma wajawazito ili wapige kura bila ya kukaa kwenye foleni.
Mabaraza ya Wazee yameanzishwa kwa kuzingatia sera ya Taifa ya wazee ya mwaka 2003, sera ya afya ya mwaka 2007 na miongozo mbalimbali lengo likiwa ni kuhakikisha wazee wanastawi vyema na kupatiwa fursa sawa pasipo kubaguliwa kwa aina yoyote.
Kwa upande wa Tanzania kupitia sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inaonesha wazee wameongezeka kufikia Milioni 2.7 ukilinganisha na Milioni 1.4 kwa mwaka 2002.
Kabla ya uzinduzi huo wajumbe wa baraza hilo walifanya uchaguzi na viongozi wa mkoa na kuwachagua Bwana Jackson Halbedi kutoka Wilaya ya Babati kuwa Mwenyekiti, Bi. Hellen Ngobei kutoka Kiteto kuwa Makamu Mwenyekiti,Bwana Elikana J. Elikana kutoka katibu, Bi Aurelia Asenga kutoka Wilaya ya Babati kuwa Katibu Msaidizi, Morandi Kunambi kutoka Mbulu kuwa Mweka Hazina,Bi. Agness Kilenga kutoka Babati Mji n kuwa Mwakilishi wa wanawake na Bwana. Paulo Gehari kutoka Mbulu kuwa mwakilishi wa wanaume.
Katika uzinduzi huo Mkuu wa Mkoa alitoa ushauri kwa wazee kutumia kauli mbiu isemayo “Tanzania ipi kwa sababu wazee wapo!! Wazee wapo kwa sababu Tanzania ipo”
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.