Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amewataka viongozi katika ngazi ya mkoa hadi vijiji kote nchini kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza darasa la saba hawaondoki katika maeneo yao kwenda kufanya kazi za ndani wakati wakisubiri matokeo ya kuhitimu darasa la saba kwani kwa kufanya hivyo kunawaondolea fursa yao ya kuendelea na masomo pindi wanapofaulu.
Naibu waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo mkoani Manyara wakati akizungumza na viongozi hao kuhusu hali ya Elimu mkoani humo ambapo amewataka kusimamia kwa ukaribu suala hilo ili kutokatisha ndoto za watoto hao na kwamba wale wanaofanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
"Hakikisheni watoto hawa wanaposubiri matokeo hawasafirishwi kwani wanapofika huko wanarubuniwa na waajiri hivyo hata matokeo yakitoka na kuonesha wamefaulu hawarejei kuendelea na masomo." Alisisitiza Naibu waziri Ole Nasha
Amesema fursa za Elimu katika nchi yetu ni kubwa kwa sasa kwa kuwa Elimu msingi ni bure hivyo hakuna kisingizio tena kuwa mtoto hawezi kusoma kwa kuwa mzazi hana fedha
"wazazi msiwe sehemu ya kuchangia watoto wenu kwenda mjini kwa kuwa tu wanawatumia fedha kwa ajili ya matuzi bali hakikisheni mnawasimamia watoto hao katika kipindi chote wanachosubiri matokeo na kuwapeleka shule pindi matokeo yanapotoka na kuonekana wamefaulu,"aliongeza Naibu waziri Ole Nasha
Amewataka viongozi hao kutumia sheria kuhakikisha watoto wenye umri wa kuandikishwa wanaandikishwa ili kutokuwa na wimbi kubwa la watoto wa mitaani wasioenda shule.
Awali Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Arnold Msuya alimweleza Naibu waziri wa Elimu kuwa mkoa huo una mwamko mdogo wa Elimu hasa katika jamii ya wafugaji hali inayopekea kutowaandikisha shule watoto wao wenye umri wa kuanza shule.
Naibu waziri Ole Nasha pia ametembelea Chuo cha Ufundi stadi VETA Manyara na kuwataka kupitia mitaala yao ili iendane na wakati, ikidhi mahitaji ya soko lakini pia wanafunzi weweze kusoma vitu vingi kwa wakati mmoja na viwe ni vile vinavyoendana na soko la ajira ili kuongeza fursa ya vijana kujiajiri pindi wanapomaliza masomo yao.
(Kwa Picha mbalimbli na Video za matukio angalia Kituo cha Habari kisha nenda Maktaba ya Picha na Maktaba ya Video)
Imeandikwa Na: Haji Athumani (Afisa Habari Mkoa wa Manyara)
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.