Naibu waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Godwin Mollel jana August 5 amefanya ziara ya siku moja Mkoani Manyara kwa kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara na kujionea shughuli mbalimbali,kuona jinsi jinsi wagonjwa wanavyopata huduma na kuongea na watumishi wa Hospitali ili kutatua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika kazi zao za kila siku katika Hospitali hiyo.
Kabla ya kutembelea Hospitali ya Rufaa Naibu waziri huyo alipokelewa na Mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe.Joseph Joseph Mkirikiti katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kisha kuendelea na ratiba yake katika Hopitali ya rufaa akiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt.Damas Kayera.
Akimkaribisha Hospitalini hapo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara Dkt. Catherine Magali alisema kuwa Hospitali inahudumia wastani wa wagonjwa wa nje 2905 kwa mwezi na wagonjwa wa kulazwa wastani wa wagonjwa 450 kwa mwezi. Pia kutokana na Mkoa kupakana na Mikoa ya Singida na Dodoma Hospitali inahudumia wagonjwa wa kutoka Wilaya za jirani za mikoa hiyo.
“Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara vilevile imekuwa na utaratibu wa kufanya huduma za kibingwa kwa mwaka mara mbili kwa kuita madakatari bingwa waliopo Mikoa ya jirani kwa kushirikiana na madaktari bingwa waliopo hapa ili kufikisha huduma kwa wananchi wenye uhitaji wa Mkoa wa Manyara na Mikoa ya jirani” Alisema Dkt. Catherine.
Akizungumzia juu ya Hospitali kutumia mifumo mbalimbali ya TEHAMA Dkt Catherine amesema kuwa Hospitali inatumia mifumo yote kama AFYA CARE, Mfumo wa Maabara (LABNET), Mfumo wa taarifa za kiutumishi (HRHIS),Mfumo wa kusajili watumishi (Biometric register), Mfumo wa GePG kwa ajii ya kukusanya mapatao pamoja na kufunga CCTV Camera kwa ajili ya usalama wa watumishi,mali za Serikai,wagonjwa na wageni wanaoingia na kutoka eneo la Hospitali.
Mara baada ya kupata taarifa kutoka kwa Mganga Mfawidhi Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt.Mollel alitembelea kituo maalumu cha kuhifadhia wagonjwa wa Covid 19 na kupewa maelezo kuwa kwa sasa hakuna mgonjwa hata mmoja katika kituo hicho kwani wagonjwa wote wamepona na kuruhusiwa.
Vilevile alitembelea Maabara ya kisasa iliyopo katika Hospitali hiyo na kuona jinsi watumishi wa maabara wanavyofanya kazi kwa bidii ili kutoa majibu vipimo vyote kwa wakati na kutembelea chumba cha upasuaji, pia alipata nafasi ya kuonana na baadhi ya wagonjwa waliokuja kupata huduma Hospitani hapo na wagonjwa hao kumweleza Mhe. Naibu Waziri wa Afya kuwa wanaridhika na huduma zinazotolewa Hospotalini hapo.
Baada ya kutembea na kujionea shughuli mbalimbali katika Hospitali hiyo Mhe.Naibu Waziri wa Afya alifanya kikao na Watumishi Hospitalini hapo na kusiliza changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo fursa ya kwenda kusoma,punguzo la riba kwenye mikopo.
Dkt.Mollel aliwatoa wasiwasi watumishi hao kwa kuwaeleza kuwa serikali itahakikisha watumishi wote wa Sekta ya Afya na sekta nyingine wanapata stahiki zao kwa mujibu wa miongozo ya serikiali na kuwaasa watumishi kuishi kwa kupendana ili kuwapa huduma bora wananchi.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara ilianzishwa Mwaka 2013 ikiwa chini ya Katibu Tawala Mkoa wa Manyara na baada ya hapo kuanzia mwaka 2018 ilihamishiwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, wazee na Watoto chini ya Katibu Mkuu kutokana na maelekezo kutoka kwa Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt John Pombe Magufuli.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.