Naibu waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe leo 3/7/2020 amefanya ziara ya siku mija Mkoani Manyara kwa kukutana na wataalam wa Kilimo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara na kutembelea mashamba ya ngano yaliyopo wilaya ya Hanang
Akimkarisha Naibu Waziri huyo Mkoani Manyara Katibu Tawala Mkoa wa Manyara Bwana Musa Missaile alisema Mkoa wa Manyara unazalisha mazao mbalimbali kama vile Mahindi,Mbaazi,Ufuta,Maharage, Pamba,Vitunguu saum,Vitunguu maji na mazao mengine katika wilaya zote tano za Mkoa wa Manyara kwa kutegemea mvua na kilimo cha umwagiliaji katika baadhi ya maeneo.Pamoja na Mkoa wa Manyara kulima mazao mbalimbali Katibu Tawala alisema Mkoa unakabiliwa na changamoto ya usafiri kwa wataalam wa kilimo ili kuweza kufika katika maeneo mengi ya Mkoa kulingana na ukubwa wa Mkoa na upungufu wa Maafisa Ugani katika ngazi za Halmashauri.
“Mheshimiwa Naibu Waziri Mkoa wa Manyara ukipata Maafisa ugani wa kutosha katika Halmashauri zetu tuna uhakika wa kuzalisha zaidi kwani kijiografia Wilaya zote za Mkoa wetu zinazalisha mazao ya aina mbalimbali kwa kutegemea mvua na kilimo cha umwagiliaji,kwa kupata Maafisa ugani kutawawazesha kwenda kwa wakulima kufundisha njia bora za kilimo na kuongeza uzalishaji” Alisema Katibu Tawala.
Akijibu hoja hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri Bashe aliahidi kuhakikisha kuwateta Mkoa wa Manyara wanafunzi wanaotarajia kufanya mafunzo kwa vitendo ili waweze kusaidia wakulima Mkoani Manyara.
“Wizara itawaletea Maafisa Ugani waliopo katika mafunzo kwa vitendo ili wawasaidie wakulima wetu lakini na nyinyi kama Mkoa muwahakikishie kuwapa huduma za malazi kwa kipindi chote watakachokuwepo Mkoani Manyara” Alisisitiza Mheshimiwa Bashe.
Mara baada ya kukuribishwa Mkoani Mheshimiwa Naibu Waziri alikwenda Wilayani Hanang na kutembelea Mashamba ya Ngano Basotu.
Mheshimiwa Naibu Waziri alipofika katika mashamba hayo alifanya ukaguzi wa mitambo mbalimbali iliyopo katika shamba hilo na kugundua upotezu wa vifaa na uvamizi wa eneo la shamba na kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Hanang na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang kushirikiana na Jeshi la wananchi kuhakikisha mashamba ya ngano Basoti yanalindwa ili kuzuia upotevu wa mitambo na uvamizi katika shamba hilo.
“ Nimeangalia shamba lina eneo kubwa na mitambo mikubwa yenye thamani kubwa sana lakini kuna baadhi ya vifaa vinaibwa katika shamba hili, hivyo nakuagiza Mkuu wa Wilaya ya Hanang na Mkurugenzi wa Halmashauri hii kushirikiana na Jeshi ili kuhakikisha usalama wa mitambo na eneo la shamba halivamiwi tena.” Alisema Mheshimiwa Naibu Waziri.
Akiwa katika shamba la SETCHET Mheshimiwa Naibu Waziri alikutana na kuongea na Mwekazaji wa shamba hilo na kumtaka Mwekezaji huyo kuhakikisha Wafanyakazi wanalipwa kwa wakati, wanapata stahiki zao kulingana na mikataba waliongia na mwekezaji wa shamba hilo.
Akihitimisha ziara hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri ameigiza Bodi ya mazao mchanganyiko kuhakikisha ngano inanunuliwa kwa bei iliyopo sokoni bila ya wakulima kukopwa na kuwataka Maafisa ugani walipo kuhakikisha wanatoe elimu ya kilimo bora, vilevile aliagiza Kampuni ya Ngano Ltd ipewe eneo la kulima kulingana na uwezo wake kwani imepewa eneo kubwa lakini hawawezi kulima eneo lote.
Ziara ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo ni muendelezo wa ziara viongozi wa Serikali ya awamu ya tano katika kuhakikisha inaleta maendeleo kwa wananchi wa Tanzania.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.