Imeandikwa Na: Haji Msovu (Afisa Habari - Mkoa wa Manyara)
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (T.F.F) Wallace Karia ameahidi kuleta mabadiliko katika soka Mkoa wa Manyara kwa kuboresha miundo mbinu ya viwanja ili kuhakikisha mechi kubwa za kitaifa zinachezwa katika Mkoa huo.
Akizungumza na waandishi wa Habari jana Mjini Babati, Rais Karia ameitaka Halmashauri ya Mji wa Babati ambao ni wamiliki wa Uwanja wa Kwaraa kuhakikisha uwanjwa huo unazungushiwa majukwaa ili Shirikisho litume wataalamu kwa ajili ya kushughulikia eneo la kuchezea.
Rais huyo amesema kwa sasa shirikisho hilo linapita kwenye mikoa ambayo ipo chini kisoka ili kuangalia uwezekano wa kuinua soka katika mikoa hiyo.
“Kuna Mikoa ambayo ipo chini Kisoka ikiwemo Mkoa wa Manyara ambapo timu ya Morani ambayo ilikuwa chini ya mikono yangu tangu ishuke daraja haijawahi kutokea timu nyingine kubwa Zaidi” Alieleza Karia
Karia amesema Uongozi wa mkoa wa Manyara kwa kushirikiana na TFF watahakikisha mkoa huo unakuwa na viwanja ambavyo vitawezesha timu kubwa kufika katika mkoa huo na kusaidia kuongeza pato la mkoa na taifa kwa ujumla.
Karia amesema ana imani kubwa na mkuu wa mkoa Joseph Mkirikiti kwa kuwa alishaonyesha nia ya kuendeleza michezo na miundombinu ya viwanja wakati alipokuwa Mkuu wa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi huku akiisaidia Majimaji ya Songea kupanda daraja.
Kwa upande mwingine Rais Karia amesisitiza kufanyika kwa program mbalimbali katika shule za Msingi na Sekondari ili kukuza soka la vijana na wanawake na kwamba wapo tayari kuleta walimu wa soka katika shule ambazo hazina walimu Pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu wa Michezo waliopo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe.Joseph Mkirikiti amewataka wafanyabiashara wote waliopewa maeneo kuzunguka Uwanja wa Kwaraa kukamilisha haraka ujenzi wa vibanda ili kuzipata fursa zilizoahidiwa na TFF.
Ikumbukwe kuwa safari ya Rais wa TFF Bwana Wallace Karia katika uongozi wa Soka ilianzia Mkoani Manyara alipokuwa Mtumishi wa Umma katika Wilaya ya Kiteto kama Mweka Hazina.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.