Na: Mariam Juma,Hanang.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Joseph Mkirikiti amemwagiza Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Hanang Solomon Isack kuwahamisha watumishi wa idara ya elimu wilayani hapo waliodumu kwa zaidi ya miaka 5 kwa kile alichokieleza kuwa hao ndio wanaokwamisha jitihada za ufalu wa watoto wilayani hapo.
Kauli hiyo ya Mkuu wa Mkoa inakuja mara baada ya wilaya hiyo kushika nafasi ya mwisho kimkoa kwa muda wa miaka mitatu mfululizo huku watumishi wa idara hiyo wakishindwa kubuni mbinu mpya za kuongeza ufaulu katika wilaya
“Nimekuja wilaya hii kama Mkuu wa wilaya hii nikakuta Hanang ni ya mwisho watumishi wa idara hiyo ni wale wale,mwaka wa pili nikiwa hapa tumefeli kama wilaya tena nikiangalia wataalamu waliopo bado ni wale wale,mwaka huu tena mmefeli watu ni wale wale nasema Mkurugezi hamisha watu hawa”alisema Mkirikiti,
Alisema ili kuhakikisha wanaongeza kiwango cha ufaulu wilayani hapo bila kuwahamisha wataalamu hao wa muda mrefu bado ni tatizo kwani hata wakiwaleta Mafisa elimu wengine wapya bila wataalamu hao wa chini yake kuhamishwa bado itakuwa ni tatizo hivyo kinachotakiwa ni kuwahamisha na kuleta wengine wapya watakaoisaidia wilaya hiyo kuongeza ufaulu na kuacha kushika nafasi ya mwisho Kimkoa kila mara.
Mkirikiti akawataka pia kuhakikisha wanakamilisha miundo mbinu ya madarasa ili wanafunzi waliofaulu waweze kuingia darasani na kuanza masomo yao.
“Mwanzoni mpaka naondoka hapa tulikuwa na upungufu wa madarasa 78 tukayapunguza yakafika 15 sasa kama yameongezeka nendeni hivyo hivyo msijipunguzie maana kule mkoani nikiwaambia nileteeni upungufu wa madarasa mnaniambia hamna upungufu wa madarasa na mnaupungufu wa madarasa 14 lakini mnatakiwa mjiwekee lengo la madarasa 30 kwasababu mnasema madarasa yanatosheleza Hanang ni kwasababu mmeendelea kuwa watu wa kufeli,hivyo kwasababu hakuna wakufaulu madarasa ndio maana yanatosha na kama wangekuwepo kugekuwa na uhitaji”alsema Mkirikiti.
Pia akamtaka Mkurugenzi kuwahamisha walimu ambao wamekuwa ni wasemaji wa walimu wenzao na wanaofanya kazi kwa mazoea kwani nao hao ni tatizo na wakwamishaji wa elimu wilayani hapo.
Naye Mkuu wa wilaya hiyo Gharibu Lingo alieleza kuwa jumla ya watoto wa darasa la saba waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza ni 4773 na wanaupungufu wa madawati 1837 pamoja na upungufu wa madarasa 30 na yanatakiwa yapatikane ifikapo January 2021.
Mkuu wa wilaya akawataka madiwani wapya walioapishwa kurudi na kujua mikakati ya kumaliza mapungufu hayo kwa kuwa mikakati ya awali ni kuhakikisha watoto waote waliofaulu wanaingia madarasani
“Madiwani rudini kwenye kamati zenu za maendeleo za kata Ili mkaweke mipango mikakati mtakayokuta wajumbe wenu wameiandaa lakini pia mboreshe na mtakapokwama tuwasiline maana sisi ni wamoja “alisema Lingo.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.