Leo Januari 16, 2024 RC Sendiga akiwa katika kijiji cha Kimotorok Wilayani Simanjiro katika ziara yake maalumu ya kikazi ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi, ametatua mgogoro uliokuwepo kati ya Wananchi wa Kijiji hicho na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na kuachia Mifugo zaidi ya 800 ikiwemo Ng'ombe, Mbuzi na Kondoo iliyokua imeshikiliwa na uongozi wa hifadhi baada ya wafugaji kuingiza mifugo hifadhini.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mkuu wa Mkoa amewaagiza viongozi wa ngazi mbalimbali kusimamia makubaliano na maelekezo ambayo yanapitishwa na Serikali au vikao na kuwaambia wananchi ukweli pasipo kuwaficha ili wapate uelewa juu ya maamuzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa ili kuepusha migogoro isiyo na tija.
Aidha, RC Sendiga ametoa maelekezo kwa uongozi wa hifadhi ya Tarangire kuwaacha Wananchi waendelee kupata huduma za mifugo yao ambazo bado zinapatikana katika hifadhini humo kama vile sehemu za kunyweshea mifugo na kuwataka wananchi hao kuendelea kutii sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa na pia kuwataka wahifadhi kujizatiti zaidi katika utoaji wa elimu na kuboresha mahusiano kati yao na Wananchi.
Sambamba na hilo RC Sendiga amewajulisha Wananchi wa Kimotorok na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha shilingi Milioni 300 kwajili ya uboreshaji wa Miundombinu ya Elimu na Afya kijijini humo.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.