Na Nyeneu, P. R - Endagaw Hanang
Mkuu wa mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga amewataka wananchi mkoani kwake kuipokea kwa mikono miwili miradi inayoletwa na serikali kwa ajili ya maendeleo yao.
Amezungumza hayo kwenye mkutano wa hadhara na wakazi wa kata ya Endagaw wilayani Hanang' uliolenga kuwahimiza wenye maeneo eneo la mradi wa Skimu ya umwagiliaji kupisha ili mradi huo uendelee kutekelezwa.
Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja ulianza kutekelezwa kijijini hapo tangu mwaka 2016 lakini umekuwa ukisuasua kutokana na baadhi ya watu wachache kuzuia utekelezwaji wa mradi na kudai kupewa fidia.
Amesema kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi, serikali ya awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha sekta ya kilimo kwa kubuni na kuanzisha Skimu za Umwagiliaji ili wakulima wafanye kilimo cha kisasa na katika misimu yote.
Mhe. Mkuu wa Mkoa ameagiza viongozi wa kijiji kufanya vikao vyao vya kisheria na kukubaliana ili fedha za mradi huo ziingie na kuanza kufanyiwa kazi kama ilivyo adhima ya serikali.
"Kule kulipojengwa skimu ya kwanza ndipo kwenye chanzo kikubwa cha maji kinachotosheleza kulisha wilaya nzima ya Hanang' ila watu wachache hao wamegoma kupisha hadi walipwe fidia ila mimi nimekuja kuwaomba mkubali ili mradi uendelee wakati taratibu zingine zinaendelea kuwatafutia maeneo mengine ya kilimo" Aliwasihi RC Sendiga.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.