Rais wa Shirika la Msalaba mwekundu Tanzania Bwana David Mwakiposa Kihenzile ameitaka kamati ya maafa mkoa wa Manyara kushirikiana na kamati uokoaji Mkoa ili kukabiliana na maafa katika Mkoa huo.
Bwana David Mwakiposa ameyasema hayo jana alipokuwa akizindua Kamati ya maafa Mkoa wa Manyara katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara kwa kuitaka kamati ya maafa kushirikiana na Kamati ya uokoaji ili kuondoa viashiria vya vya maafa,kutoa elimu na taahadhari ya maafa na kushiriki kikamilifu kusaidia waliokumbwa na maafa.
“Tunataka kila Kijiji na kila shina kuwe na mtu wa kujitolea ili yakitokea maafa aweze kusaidia na kwa kuwa tumetoa mafunzo kwa watu 40 wa kamati ya uokoaji wakiwemo wenzetu 10 wa Jeshi la zima moto ili kuhakikisha elimu ya kukabiliana na maafa inafika katika ngazi zote!!” Alisema Rasi huyo wa Red Cross.
Akielezea jinsi Shirika hilo la Msalaba Mwekundu Tanzania lilivyofanya kazi kubwa Mkoani Manyara Bwana Mwakiposa alisema kuwa shirika hilo lina mradi mkubwa wa ujenzi wa Mabwawa katika Wilaya ya Simanjiro na katika katika Wilaya ya Kiteto wanatoa elimu juu ya usalama wa chakula na jinsi ya kutumia mbegu bora.
Pamoja na kuzindua uzinduzi wa kamati ya uokoaji Mkoa wa Manyara Rais huyo wa Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania pia aligawa vifaa mbalimbali vya kukabiliana na maafa kama vile Machela 5, Maturubai ma 3, Vikoi vya kuvaa wakati wa kukabiliana na maafa na bendera zenye nembo ya Msalaba mwekundu.
Akizungumzia changamoto zinazolikabili Shirika hilo, Rais wa Red Cross alisema kuwa changamoto kubwa ni uelewa wa wananchi juu uelewa wa kazi za shirika hilo kwani wananchi wengi wanadhani Red Cross ni wanyonya damu lakini wanaendelea kutoa elimu ili jamii iondokane na dhana potofu, changamoto nyingine ni ukosefu wa ofisi za kudumu za shirika hilo kuanzia ngazi za wilaya na mikoa.
Akiongea wakati wa kumkaribisha Rais wa Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania Mwenyekiti wa Shirka hilo Mkoa wa Manyara Bwana Moses John Basila ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Manyara kwa kuwapatia Ofisi ya Mkoa katika Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa bila malipo yoyote ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
“Mheshimiwa Rais napenda kuchukua nafasi hii kuushukuru uongozi wa Mkoa wa Manyara ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa Mhe.Joseph Mkirikiti na Katibu Tawala Mkoa Bwana Musa Missaile kwa kutupa Ofisi bila kulipia gharama zozote, hii inaonesha jinsi gani viongozi hawa walivyo kuwa na ufahamu juu ya Red Cross” Aliongeza Mwemyekiti wa Red Cross Mkoa wa Manyara
Akitoa Shukrani zake kwa Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania Katibu Tawala Mkoa wa Manyara Bwana Musa Missaile amesema kuwa amefurahishwa na jinsi Shirika hilo linavyofanya kazi zake katika Mkoa wa Manyara kwa kuanza na kujenga miradi ikubwa katika wilaya za Simanjiro na Kiteto na kuahidi kulipa shirka hilo ushirikiano wa hali ya juu wakati wowote na pia kutoa ahadi ya kuhakikisha Shirka linapata maeneo ya kujengea ofisi katika Halmashauri zote saba za Mkoa wa Manyara.
“Katika kuhakiksiha mnaondokana na tatizo la kuwa na Ofisi sisi kama Mkoa tutawaelekeza Wakurugenzi wote wa Halmashauri wawapatie maeneo ili muweze kujenga ofisi zenu ili elimu juu ya kazi za Shirika la Msalaba Mwekundu ziwafikie wananchi wetu wa Manyara kila mahali” Alisema Katibu Tawala Mkoa wa Manyara.
Akishukuru kwa niaba ya washirkiki wa mafunzo kwa kamati ya maafa Mkoa wa Manyara Mama Annah Ufoo (maarufu kwa jina la Mama Ango) kutoka kwa wafanyabiashara wa sekta binafsi alisema kuwa yeye kama mfanyabiashara amenufaika san ana mafunzo hayo na atakwenda kuwaelimisha wafanyabiashara wenzake kupata elimu juu ya majanga na kukabiliana na majanga.
“Kuna haja ya Shirika hili la Msalaba mwekundu kutoa elimu kwa wananchi ili watu wengi wajiunge na mimi binafsi nitawashawishi wafanyabiashara wenzangu ili tuisaidie Red Cross kuwezesha mafunzo ya mara kwa mara kwetu na wananchi wote wa Mkoa wa Manyara kuanzia shule za msingi mpaka mitaani” Alisema Mama Ango.
Shirika la Msalaba Mwewkundu Tanzania limeanzishwa kwa sheria namba 7 ya Mwaka 1962 ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria ya maafa namba 7 ya Mwaka 2015 likiwa na majukumu ya kueneza kanuni na maadili ya kibinadamu ,kutoa misaada katika hali za dharura kwa kipimo kikubwa ,kusaidia Vyama vya kitaifa katika kujitayarisha ili kukabiliana na majanga kupitia elimu kwa wanachama wake wa kujitolea na utoaji wa vifaa na vifaa vya kutoa msaada, kusaidia miradi ya afya kwa mitaa, kusaidia vyama vya kitaifa katika shughuli zinazohusu vijana.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.