Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni tisa kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji Mkoani Manyara ambapo kwa kila Mkoa umetenga Wilaya Shilingi Bilioni 1,366,865 na kwa Wilaya ya Simanjiro imepanga kutekeleza miradi sita iliyopo Wilayani humo ili kuhakikisha wananchi wa Wilaya hiyo wanaepukana na kero za kutafuta maji be kwa kutembea umbali mrefu.
Hayo yamesemwa jana na Meneja wa RUWASA Mkoa wa Manyara Mhandisi Wolta Kirita wakati wa ukaguzi wa miradi ya Maji uliofanywa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Joseph Mkirikiti na Kamati ya siasa Mkoa wa Manyara Wilayani Simanjiro katika kuhakikisha kauli ya Mhe.Rais John Pombe Magufuli ya kumtua Mwanamke ndoo kichwani inatimia kwa kuhakikisha wananchi hawatembei umbali mrefu kutafuta maji.
"Mheshimiwa Waziri Mkuu Mstaafu kwa kipindi cha mwezi Oktoba 2019 hadi 2021 RUWASA imejipanga kuhakikisha inamalizia miradi sita ya maji iliyopo katika Vijiji vya Oljoro namba 5,Narakauo,Longswan-Terrat,Komolo,Shambai-Kilombero na Emboreet ambapo tunatarajia kuwanufaisha wakazi 15,246 watanufaika na mradi huu kwani tutajenga vituo 47 vya kuchotea maji"Alisema Mhandisi Kirita.
Pamoja na mradi huo wa Longswan Mheshimiwa Waziri Mkuu Mstaafu na Viongozi alioambatana nao walitembelea mradi mkubwa wa Ruvu-Remit unaogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 40 unaondelea kunajengwa katika mji wa Orkesumet.Mara baada ya kukamilika kwa mradi huo wananchi wa Simanjiro,Mirerani,Kiteto,na baadhi ya Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro pia watanufaika na maji kwa mradi huo una uwezo wa kuhudumia watu wengi kuliko idadi ya wananchi waliopo Wilayani humo.
Pia Viongozi hao walitembelea mradi mwingine wa maji wa Londrekes.
Pamoja na kuridhishwa na miradi hiyo mara baada ya Viongozi hao kukagua na kujionea maendeleo ya miradi hiyo Viongozi hao waliwataka Viongozi katika ngazi za Vijiji na Kata wawe wasimamizi wakubwa juu wa wananchi wanaohujumu miundombinu ya maji inayofanywa katika maeneo yao ya utawala.
"Kiukweli sisi kama Viongozi tumekagua miradi hii na tumeridhika nayo ila napenda kuwaambia Viongozi wenzangu katika ngazi za Vijiji na Kata kuhakikisha mnalinda miundombinu hii ili isiharibiwe kwani Serikali inatumia fedha nyingi sana kuwekeza katika miradi ya maendeleo ili wananchi wake wapate huduma nzuri, sasa hakikisheni mnawabaini wote wanaohujumu miundombinu ya maji na mingine na kuwachukulia hatua kali za kusheria" Mhe. Joseph Mkirikiti.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Mizengo Pinda alifurahishwa na jinsi RUWASA wanavyojitahidi kuhakikisha wanapelea huduma za maji kila kona na kuwataka wakala hao kuwa kama Shirika la Umeme linavyopeleka umeme kila kona.
"RUWASA pamoja na kazi nzuri mnayofanya mnatakiwa kuhakikisha mnawafikishia maji wananchi kila mahali kama wanavyofanya Tanesco katika umeme". Alisisitiza Mhe.Pinda.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara na kamati ya Siasa Mkoa wanaendelea na ziara yao ya kukagua miradi ya maji inayotekelezwa na wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) katika Wilaya zote za Mkoa huo ili kuhakikisha wananchi wa Manyara wanaepukana na kero za kutafuta maji kwa kutembea umbali mrefu.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.