Wakala wa Maji Vijijini RUWASA mkoa wa manyara imewahakikishia wakazi wa kata ya Inkaiti,Wilaya ya Babati katika Mkoa wa Manyara kuwa itamaliza shida ya upatikanaji wa maji safi na salama katika kata hiyo ifikapo mwezi Novemba 20, 2020 mara baada ya mradi mkubwa (Mayoka- Minjingu) wa kusafirisha maji wenye thamani ya zaidi shilingi bilioni mbili kutoka Kijiji cha Mayoka kwenda Minjingu kumalizika.
Akizungumza leo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe.Joseph Mkirikiti Meneja wa RUWASA mkoa wa Manyara Mhandisi Wolter Kirita amesema kuwa watatumia jumla ya shilingi bilioni moja na nusu kwa ajili ya kununulia mabomba na kati ya milioni mia nne mpaka mia tano itafanya kazi nyingine ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kati ya shilingi bilioni mbili walizipokea kwa ajili ya mradi huo wa Myoka- Minjingu.
“Pale kazi kubwa ni kuyalaza mabomba kwenye ziwa Manyara na tunaanza kulaza bomba hizo Ijumaa kwa kuwa upande wa mayoka tumeshalaza, kwa hiyo tukimaliza kulaza bomba kazi itakuwa imeisha na wananchi wa Kata ya Nkaiti wataanza kupata maji kuanzia mwezi Novemba mwaka huu” Alisema Mhandisi Wolta.
Pamoja na kufikisha maji katika kati hiyo ya Nkaiti Meneja huyo wa RUWASA amesema kuwa awamu ya pili ya mradi ni kuhakikisha maji yanafika katika kituo cha Afya Nkaiti ifikapo mwezi Januari 2021 ili kuwaondolea kero ya waji wananchi mbalimbali wanaopata huduma za afya katika kituo hicho.
“Baada ya kupeleka maji Minjingu tutaongeza mkondo wa maji kutoka Minjingu kwenda kwenye Kituo cha Afya cha Nkaiti ifikapo mwezi Januari kupitia mradi wa PBR4” Aliongeza Meneja huyo wa RUWASA Manyara.
Mara baada ya kukagua mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe.Joseph Mkirikiti aliwapongeza wafanyakazi wa RUWASA mkoa wa Manyara kwa juhudi zao za kuhakikisha wananchi wa Kata ya Nkaiti wanapata maji haraka na kuwataka kufanya kazi usiku na mchana ili maji yafike kwa wakati.
“Kwa kweli ni kitu kizuri kinachofanyika ili kuhakikisha tunapeleka maji kwenye zahanati, Vituo vya afya,Shule na kwenye mikusanyiko ya watu wengi ili na hakika mimi binafsi navutiwa na utendaji kazi wa RUWASA katika Mkoa wa Manyara”Alisema Mhe.Mkirikiti.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Manyara Bwana Musa Missaile amezishukuru Halmasahuri za Mji na Wilaya ya Babati kwa kuwaazima boti RUWASA ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi hasa zile kazi za kuhakikisha wanavusha bomba kukatiza ziwa Manyara kwenda katika Kijiji cha Mayoka.
“Nazipongeza sana Halmashauri zote mbili za Mji na Wilaya ya Babati kwa kuwaazima boti RUWASA ili kuhakikisha wenzao wanafanya kazi hii kwa haraka ili wananchi wa Nkaiti waanze kupata maji katika kwa wakati uliopangwa” Alisema Katibu Tawala.
Wakionesha furaha zao mbele ya Mkuu wa Mkoa wananchi wa Minjingu wamesema kuwa wataunda kamati mbalimbali za kulinda miundo mbinu ya maji katika mradi huo ili isiharibiwe na watu wasiowatakia mema kwani mradi huo utawasaidia kuepukana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata maji.
“Yaani Mheshimiwa Mkuu wa tunakuhakikishia tutalinda mradi huu kwa gharama zote ili wasije kuhujumu tukakosa maji kwani baada ya kuanza kupata maji hata wake zetu watapunzika na kutembea umbali mrefu kufuata maji na kule kwenye Kituo cha Afya tutaacha kwenda na vidumu na ndoo za maji kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa” Alisema bwana Joseph John Mkazi wa Minjingu.
Kukamilika na Mradi huo wa maji wa Mayoka -Minjingu kutaondoa kero ya muda mrefu iliyokuwa inawakabili wakazi wa Kata ya Nkaiti kutokana na changamoto ya kupata maji maji yenye magadi katika eneo hilo na hivyo kutofaa kwa matumizi ya bidamu.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.