Waziri wa nchi ,Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh.Januari Makamba (Mb) alifanya ziara Katika Mkoa wa Manyara na kutembelea Halmashauri ya Mji wa Babati tarehe 6/9/2018 na kuongea na viongozi pamoja na wananchi juu ya uhifadhi wa ziwa babati.
Akiongea na viongozi waziri Makamba alisema "Dhumuni la ziara yangu ni kuhakikisha sifa ya Tanzania inabaki katika uhifadhi wa rasilimali kwa ajili ya kizazi kijacho na pia ipo fursa ya kuyatunza na kuyahifadhi maeneo yetu lindwa yaliyopendekezwa na Mkoa wenu kwa kutumia sheria ya mazingira”.
Aidha waziri Makamba alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Manyara kuteua kikundi cha maafisa au wataalam wa mazingira ili wakapate mafunzo juu ya uhifadhi wa mazingira ,pia alizitaka Halmashauri kuungana na (NEMC) ili kukasimu kazi zake katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika kukusanya ada kama chanzo cha mapato vilevile alisema huduma za kiikolojia zinaweza kuufanya Mkoa kunufaika na huduma za kiutalii na pia alitoa rai kwa viongozi sheria ndogo za kimazingira zibadiliswe mfano sheria ya ndogo ya Halmashauri ya Mbulu ya uhifadhi wa mazingira ya Mwaka 2004.
Katika mkutano wake na wananchi wa kijji cha Himiti katika Kata ya Bonga Halmashauri ya Mji wa Babati Mh. waziri alisema ziwa Babati lina nafasi kwa ustawi wa maendeleo ya watu wa Babati zipo changamoto zinazolikabili ziwa hilo” ni mezungumza na mwenyekiti wenu kaniambia samaki wamepungua na hii ni kutokana na kina cha maji kupungua, tope limeongezeka na magugu yanazidi kuota hivyo ikifika miaka kumi na tano litatoweka kabisa” alisisitiza.
Mapendekezo yaliyotolewa na Mkoa wenu ziwa hili lihifadhiwe katika mambo ya kimazingira ni lazima wananchi washirikishwe kama kifungu cha 178 cha sheria ya mazingira kinavyosema “Umma una haki ya kupata taarifa muafaka kuhusu kusudio la mamlaka za kiutawala kuhusu mazingira” ,hivyo basi kila mwananchi ni mdau wa mazingira na ana haki ya kushitaki kwa niaba ya mazingira na maslahi ya watu yatazingatiwa kwa watu wote.
Halikadhalika Mh. Waziri alitoa fursa kwa wananchi kuchangia maoni yao kupima na kutathimini juu ya utayari wa wananchi katika mpango wa serikali unaolenga kulifanya ziwa Babati kuwa eneo lindwa ambapo wananchi hao walisema ”ziwa hili ni kama ajira kwetu hivyo Mh. Waziri mimi siipingi hoja yako kwani umeileta kwetu kwa ajili ya maslahi yetu hivyo tunakubaliana na hoja ya uhifadhi wa ziwa letu kwani asilimia kubwa ya sisi wa kazi wa hapa kazi zetu ni uvuvi kilimo na ufugaji” alisema Ayubu Gwangway
Kwa sababu mimi mwenyewe kama mkereketwa mmojawapo naunga mkono hoja ya uhifadhi wa mazingira kwani ziwa hili mkiliwekea mikakati madhubuti na sheria za kiuvuvi samaki wataongezeka na sisi kama wananchi tutanufaika kwa kutupatia kipato cha familia kwani kazi zetu sisi ni uloezi wa samaki ambao hutupatia fedha kwa ajili ya kusomeshea watoto wetu” alisisiti za Asha Hussein mkazi wa kijiji hicho.
Vilevile mkazi mwingine alisema sheria zinasaidia kutupeleka kwenye mafanikio kwani uvuvi haramu umekuwa gumzo,kilimo kisicho cha mpangilio kimechangia sana tope kujaa ziwani hivyo suala hili tumelikabidhi kwenu Serikali kwa ajili ya uhafidhi wa ziwa letu kwa ajili ya kuchangia pato la serikali.
Kutokana na maoni hayo ya wananchi Mh.Waziri Makamba alisema ameyapokea maoni hayo kwa mikono miwili hivyo nitayafikisha kwa viongozi wenzangu na nitatuma timu ya wataalam kuja kufanya uchunguzi kuweka mipaka na sheria zitakazowaongoza katika uhifadhi. Akifunga kikao mwenyekiti wa kijiji Cha Himiti wao kama wananchi wanaungana na Serikali katika kulihifadhi ziwa kwa malengo ya Taifa na kizazi kijacho na tuko tayari kutoa ushirikiano kwa watalam na Serikali katika kuyatunza mazingira yanayotuzunguka kwa ujumla pamoja na uhifadhi wa rasilimali tulizonazo.
(Kwa Picha mbalimbali angalia Kituo cha Habari kisha nenda Maktaba ya Picha)
Imeandikwa na Isabela Joseph (UDSM-Mafunzo kwa Vitendo)
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.