Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga ameagiza Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya kuendelea kusimamia taaluma kwa kuzingatia ufaulu wa wanafunzi pamoja na ujenzi wa miradi ya elimu na usimamizi wa fedha zote za sekta ya elimu nchini.
Mhandisi Nyamhanga ameyasema hayo wakati wa ziara yake mkoani Mwanza jana wakati akikagua miradi ya maendeleo sekta ya elimu, katika Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela ambapo akiwa katika shule ya sekondari Nyegezi na Fumagila zilizopo Jijini Mwanza na katika shule ya sekondari Kayenze na shule ya msingi Isenga D zilizopo Manispaa ya Ilemela amewaagiza watendaji hao kusimamia taaluma na kuzingatia matumizi sahihi ya fedha za elimu ili kuondokana na hoja za ukaguzi.
“Maafisa Elimu wote muendelee kusimamia ufaulu na taaluma na fedha zote za miradi ya elimu kama EP4R (Lipa Kulingana na matokeo), EQUIP T na fedha zote zinazotolewa na Serikali kila mwezi, hakikisheni zinatumika kulingana na kazi iliyopangwa na kwa kuzingatia thamani ya fedha halisi na kuepuka hoja za ukaguzi” alisema Mhandisi Nyamhanga.
Nyamhanga amesema Serikali inatoa fedha za Elimu Bila Malipo kila mwezi kiasi cha shilingi bilioni 23.7 kama sehemu ya malengo ya Serikali ya Chama Tawala kugharamia elimu ili kuhakikisha watoto wote wa kitanzania wanapata elimu bila kulipia kuanzia ngazi ya chekechea, shule ya msingi hadi shule ya sekondari kidato cha nne.
Aidha, Mhandisi Nyamhanga amesema Serikali inafanyia kazi suala la ajira mpya za walimu hasa masomo ya sayansi ili kupunguza uhaba wa walimu wa sayansi na pia Ofisi ya Rais TAMISEMI itapeleka fedha kiasi cha shilingi milioni 90 katika shule ya sekondari Fumagila na milioni 90 katika shule ya sekondari Nyegezi kwa ajili ya kujengea jengo la utawala.
Kwa upande wake Mkuu wa shule ya sekondari Fumagila mwalimu Victor Lyambogo amesema wamepokea kiasi cha shilingi 66.3 milioni kwa ajili ya kujengea madarasa matatu na matundu sita ya vyoolakini bado wanaupungufu wa matundu 30 ya vyoo na jengo la utawala.
Doto Boki mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari Nyegezi amesema bado wanakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa, vitabu vya masomo ya sayansi na madawati kutokana na ongezeko la wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza mwaka 2019.
Lengo la ziara ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga mkoa wa Mwanza na Mara ni kujitambulisha kama Mtendaji mpya pia kufuatilia na kukagua miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na vituo vya afya, zahanati na hospitali za wilaya, ukarabati na ujenzi wa barabara zilizo chini ya TARURA na TSCP, ujenzi wa shule za msingi na sekondari.
Imeandikwa Na: Fred Kibano
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.