Serikali imewataka wazazi wenye watoto wanaosoma shule binafsi ambao watoto wao wamelazimishwa kurudia darasa kwa kigezo kuwa hawajafikia wastani wa ufaulu wa shule hizo wapeleke malalamiko yao kwa Wakurugenzi wa Halmashauri ili yafanyiwe kazi kwani kitendo hicho ni kinyume na mwongozo uliotolewa na serikali.
Aidha alisema kuwa ili mtoto aweze kuruhusiwa kukariri darasa ni lazima mzazi aridhike na uamuzi huo kwani kitendo cha kuwalazimisha wazazi ni kinyume cha mwongozo na maagizo ya serikali.
Agizo hilo limetolewa jana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Mwita Waitara wakati akifungua mafunzo elekezi ya siku mbili kuhusu utekelezaji wa programu ya lipa kulingana na matokeo katika sekta ya elimu yanayofanyika jijini Dodoma.
Alisema kuwa hakuna sababu kwa mwanafunzi kulazimishwa kukariri darasa ikiwa alifaulu mitihani yake ya darasa la nne na kidato cha pili kwani mitihani hiyo ndiyo pekee inayoruhusiwa na serikali kupima uwezo wa mwanafunzi husika kuendelea na masomo ya juu.
“Nimekuwa napata malalamiko mengi kutoka kwa wazazi kuhusiana na jambo hili, na kama kuna mzazi anasema motto wake amelazimishwa kurudia darasa aende ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri husika ili malalamiko yake yaweze kushughulikiwa,” alisema na kuongeza:
“Haiwezekani mtoto afaulu mtihani wa kidato cha pili, cha tatu, lakini pale tu anapofika kidato cha nne baadhi ya wamiliki wa shule huwalazimisha watoto hao kurudia darasa au huwataka wafanye mtihani wa kidato cha nne lakini wajiandikishe kama watahiniwa binafsi ndipo waruhusiwe kuendelea na masomo katika shule hizo,” alisisitiza Naibu Waziri.
Kwa mujibu wa Mhe.Wazitara, mtindo huu unaofanywa na baadhi ya wamiliki wa shule binafsi umekuwa ni kero kubwa kwa wazazi wenye watoto wanaokumbwa na kadhia hiyo kwani wazazi wamekuwa wakilazimika kulipa ada mara mbili ili watoto wao waweze kuruhusiwa kuendelea na masomo katika shule hizo.
Naibu Waziri aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia ilikwishatoa mwongozo kuhusu suala hilo na kwamba walimu wanaotakiwa kufundisha katika shule wanatakiwa wawe ni wale wenye sifa zinazostahili.
Pia aliwataka waajiri wa shule hizo kuhakikisha kuwa walimu wanaofundisha katika shule hizo wana mikataba ya ajira na pia makato yao ya kila mwezi yapelekwe kwenye mifuko ya jamii.
Jambo lingine alilolitolea ufafanuzi Naibu Waziri ni suala la Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kuwa wanasimamia fedha za halmashauri ili zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.
Mhe.Waitara alionya kuwa ni marufuku kwa fedha za miradi ya elimu kutumiwa kufanya shughuli nyingine kinyume na maelekezo ya serikali.
“Kama Mkurugenzi unataka kubadilisha matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu ni lazima uwasiliane na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa ajili ya kuomba idhini ya kufanya hivyo,” alisema.
Kuhusu kuhakikisha ubora wa elimu katika shule, Naibu Waziri alitaka Maafisa Elimu Kata kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao vizuri kwani bila watendaji hao kuwajibika ipasavyo katika kata zao, maendeleo ya elimu katika ngazi hizo yataendelea kuwa duni.
Aliongeza kuwa changamoto za elimu zipo za aina nyingi ambapo licha ya walimu kuwa na sifa za kufundisha lakini kama hawawajibiki ipasavyo maendeleo ya shule lazima yatakuwa chini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Elimu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa bwana Julius Nestory aliwataka watendaji hao wa elimu katika halmashauri kuhakikisha kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya elimu zinatumika kwa shughuli husika.
Aliongeza kuwa serikali hivi sasa haitamvumilia mtendaji yeyote yule wa halmashauri ambaye atatumia fedha za serikali kinyume na maelekezo na kutoa onyo kwa waweka hazina watakao wapotosha wakurugenzi wa halmashauri kuhusu jambo hilo.
Mafunzo hayo elekezi kuhusu utekelezaji wa program ya lipa kulingana na matokeo katika sekta ya elimu yanafanyika kwa Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisaelimu wa Mikoa, Wadhibiti Wakuu Ubora wa Shule wa kanda, Maafisaelimu msingi na Sekondari, na Wadhibiti Wakuu Ubora wa Shule wa Wilaya kutoka halmashauri za mikoa ya Morogoro na Dodoma.
Programu ya Lipa kulingana na Matokeo ilizinduliwa mwezi septemba, 2014 chini ya mpango wa Matokeo Makubwa sasa kwa lengo la kuinua ubora wa elimu nchini. Kupitia program hiyo fedha hutolewa kwa kukidhi vigezo vilivyokubalika baada yua kufanyiwa uhakiki na kuthibitika.
Tangu kuanza kutekezwa kwa program hii mwaka 2014/2015 Mamlaka za Serikali za Mitaa zilipokea shilingi bilioni 15.53, na mwaka 2015/2016 jumla ya shilingi bilioni 22.36 na mwaka 2016/2017 jumla ya shilingi bilioni 40.09 zilipokelewa.
Na: Mathew Kwembe
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.