Hifadhi ya Taifa ya Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii umezindua Utekelezaji wa mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Vijiji vinavyopakana na hifadhi za Taifa ili kupunguza migogoro ya matumizi ya Ardhi.
Mpango huo ambao unalengo la kutatua migogoro ya Ardhi kati ya wananchi na Hifadhi utakaoshirikisha Mikoa mitano ya Manyara, Dodoma, Mara, Arusha na Simiyu iliyozungukwa na hifadhi za Taifa umewakutanisha Viongozi wa Mikoa hiyo leo Mkoani Manyara ili kuzindua na kujadili utekelezaji wa Mpango huo.
Aidha Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi Willium Lukuvi na Naibu waziri Maliasili na Utalii Japhet Hasunga ambapo Waziri Lukuvi aliwataka wakurugenzi wa a Halmashauri za Mikoa hiyo husika kusitisha kupeleka maombi Tamisemi ya kugawanywa kwa vijiji vipya mpaka migogoro iliyopo itakapo tatuliwa.
Alisema Migogoro mingi iliyopo ni kutokana na vijiji vipya kuanzishwa kiholela na watu wenye maslahi yao binafsi kwa mambo ya siasa na tamaa za madaraka bila kujua kuwa wanaiingizia serikali hasara ya kutumia fedha nyingi pale wanapoingia kwenye migogoro.
Waziri Lukuvi alisema Tanzania inayo maeneo makubwa ya Ardhi ila ukubwa huo hautokuwa na manufaa kama matumizi yake hayatozingatia matumizi bora ya Ardhi ambayo yatakuwa yakiwanufaisha Wananchi na kutenga maeneo ya Wakulima, wafugaji , na maeneo ya hifadhi.
Alisema Wafugaji wengi wanahitaji maeneo makubwa kwaajili ya malisho ya mifugo yao na hiyo ndio sababu ya Wafugaji kuvamia maeneo ya misitu ya Hifadhi, kutokana na hali hiyo imeleta migogoro mikubwa kati wa Wafugaji na wahifadhi misitu, migogoro ambayo inachochewa na uharibifu wa mazingira na upotevu wa uwezo wa Ardhi kuzalisha ,kufungwa kwa shoroba za wanyamapori wanapohama , na kuongezeka kwa ukame.
"Ili kuondoa migogoro hii Wizara na Taasisi imeamua kwa makusudi kuandaa mipango na matumizi bora ya ardhi, upimaji ambao utawashirikisha wananchi na Wizara zote husika, mipango hii ikifanikiwa wananchi wengi watakuwa na maendeleo makubwa
Aidha Waziri Lukuvi alisema sababu nyingine ya migogoro hii ni Wizara husika za Tamisemi, Maliasili na utalii, na Ardhi kutokaa pamoja na kupishana wanapotekeleza majukumu yao ya kugawanya vijiji na kuweka mipaka katika meneo ya hifadhi hivyo baadhi ya vijiji kuanzishwa katika maeneo ya hifadhi na maeneo ya hifadhi kuanzishwa kwenye maeneo halali ya vijiji.
"Migogoro hii huanzia wizarani kwa kutokukaa pamoja na kupanga kwani kwa kutokujua Serikali ilianzisha makazi katika maeneo ya Hifadhi kwa kugawanya vijiji na kuna maeneo Serikali imepeleka mpaka shule na Umeme bila Kujua kuwa eneo lile ni la hifadhi, sasa tukienda pale kuwafukuza wananchi hawawezi kutuelewa Sasa tunawachanganya wananchi kwasababu Wizara hizi husika hazishirikiani na kufanya kazi pamoja" alisema Lukuvi.
Aliwataka Viongozi wa Mikoa hiyo kutoa ushirikiano ili kufanikisha adhma hiyo ya Hifadhi ya Taifa ya Tanzania na Wizara ya Maliasili kutekeleza mipango wa matumizi bora ya Ardhi kwa kuwafahamisha na kuwapa elimu juu ya Nia ya na sababu za kuhifadhi maeneo ya wanyama.
Kwa Niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Tanzania Meneja Ujirani kwema hifadhi za Taifa Tanzania Ahmed Mbugi alisema sababu ya kufanya uzinduzi huo ni kutokana na ongezeko kubwa la migogoro siku hadi siku ambao unapelekea kutokuwa na ushirikiano mzuri kati ya Hifadhi na wananchi na Wafugaji na Hifadhi.
Alisema mpango huo umelengwa kufanywa tatika hifadhi 16 zilizopo Tanzania lakini kwa sasa utekelezwaji utaanza katika Mikoa ikiyozunguka Hifadhi tatu za Manyara, Serengeti , Tarangire ambao utahusisha vijiji 95 kati ya vijiji 392 vinavyolengwa.
Naibu waziri Maliasili na Utalii alisema ili kuwepo kwa matumizi bora ya ardhi ambayo hayatoleta migongano kati ya wananchi Hifadhi na Serikali yake lazima viongozi wa Mkoa,Wilaya, viongozi wa vijiji na wataalamu wa ardhi washirikishwe katika uwekwaji wa Mipaka.
"Tulikuwa tumeagizwa sisi kama Wizara ya maliasili na utalii kwamba hifadhi zetu zote na mapori tengefu tuweke mipaka inayoeleweka kwa kuweka bikon na zoezi hilo wakati linaanza halikuwa zoezi shirikishi ambalo limeleta migogoro katika maeneo mengi" alisema Hasunga.
" Sasa kama Wizara tumekaa tumeona lazima tuzingatie sheria na maelekezo, sisi kama Wizara ya Maliasili na utalii ni wahitaji wa Ardhi na wananchi ni wahitaji wa ardhi, hivyo sisi hatuwezi kuonyesha mipaka mwenye mamlaka ya kuonyesha mipaka ni Wizara ya Ardhi wao pekee ndio wanaweza kutuambia kwa Ramani hii Mipaka yetu inaishia wapi" alisema.
Aliongeza kuwa Moja ya njia ya kutatua migogoro ni kuwa na Mpango shirikishi wa matumizi bora ya ardhi, ili kutofautisha ardhi ya wanyamapori, ya wakulima, na ya Wafugaji na hivyo kuwaachia Wizara ya Ardhi kuonyesha mipaka halali kwani wao pekee ndio wenye Ramani na wanaweza kuonyesha mipaka halali.
(Kwa picha mbalimbali na video angalia sehemu ya Kituo cha Habari kisha nenda Maktaba ya Picha na Maktaba ya Video)
Imeandikwa na: Haji A.Msovu (Afisa Habari Mkoa wa Manyara)
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.