Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo kwenye Kata 79 za Tanzania Bara.
Akitangaza kufanyika kwa uchaguzi huo Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji (R), Semistocles Kaijage amesema kuwa uchaguzi huo utafanyika Agosti 12 mwaka huu na fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kuanzia tarehe 8 hadi 14 mwenzi huu (Julai).
"Uteuzi wa Wagombea utafanyika tarehe 14 Julai, mwaka huu. Kampeni za Uchaguzi zitafanyika kati ya tarehe 15 Julai, hadi tarehe 11 Agosti, mwaka huu na siku ya uchaguzi itakuwa ni tarehe 12 Agosti mwaka huu,” amesema Jaji Kaijage.
Jaji Kaijage amebainisha kuwa Tume ilipokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana akiitaarifu juu ya uwepo wa nafasi wazi za Udiwani katika Kata 79.
“Tume imepokea Taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaaa mbaye kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, aliitarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika Kata 79 za Tanzania Bara,” amesisitiza Jaji Kaijage.
Ametoa wito kwa vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi cha Uchaguzi mdogo.
Jaji Kaijage amefafanua kuwa kuwa uchaguzi huo mdogo utafanyika ndani ya Halmashauri 43 zilizopo kwenye Mikoa 24 ya Tanzania Bara.
Mikoa hiyo ni pamoja na Manyara, Kigoma, Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kagera, Katavi, Kilimanjaro, Lindi, Mara, Mbeya, Mtwara, Morogoro, Mwanza, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Singida, Songwe, Tabora na Tanga.
Kwa upande wa Halmashauri zitakazokuwa na Uchaguzi ni Babati, Moshi, Ruangwa, Mbulu, Hanang, Serengeti, Tarime, Kyela, Mtwara, Newala, Kilombero, Kilosa, Kwimba, Makete, Wanging’ombe, Kalambo, Songea, Msalala, Meatu, Singida, Songwe, Tunduma, Tabora, Nzega, Urambo na Tanga.
Halmashauri nyingine ni pamoja na Karatu, Longido, Arusha, Ngorongoro, Monduli, Meru, Ubungo, Kondoa, Mpwapwa, Chamwino, Iringa, Kyerwa, Misenyi, Muleba, Nsimbo, Kasulu na Same.
Imeandikwa na: Haji A.Msovu(Afisa Habari Mkoa wa Manyara)
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.