Imeandikwa Na: Mohamed Hamad
Waandishi wa habari mkoani Manyara wamepatiwa mafunzo ya namna ya kuandika habari za magonjwa ya mlipuko ukiwemo Covid 19.
Mafunzo hayo yamefadhiliwa na umoja wa vilabu vya waandishi wa habari nchini UTPC kuwezesha waandishi wa habari kuwa na uelewa wa kuandika habari za magonjwa ya maambukizi kwa usahihi
Afisa afya mkoa wa manyara, Evance Simkoko akifundisha mada kuhusu mzunguko wa ueneaji wa magonjwa alitaja aina mbalimbali za magonjwa na njinsi mzunguko wa maambukizi ya magonjwa hayo ulivyo na kuwataka waukate mzunguko huo kuzuia ueneaji.
Alisema mwandishi wa habari anayeandika habari za afya anatakiwa kufahamu aina za magonjwa na namna yanavyoambukizwa kwa usahihi ili atoe elimu kwa umma.
"Mwandishi anatakiwa kufahamu visababishi vya magonjwa,sehemu magonjwa yanapoishi,njia za magonjwa hayo kutoka,kukohoa ama kupiga chafya, Njia ya ugonjwa unavyosambaa,sehemu ya kuingilia mdudu kutokana na ugonjwa kwa mnyama ama binadamu aliye hatari kupata ugonjwa.
Kwa upande wake mwaandishi wa habari mwandamizi, Musa Juma aliyefundisha namna ya kuandika habari ya magonjwa ya mlipuko aliwataka waandishi hao kuwa makini na habari zinazohusu utaalamu kuwa wawe wanapata kutoka kwa vyanzo sahihi.
"Waandishi andikeni habari kwa misingi ya sheria, ukweli na usahihi wa habari kuepuka ukakasi na uchochezi ambao kuna sheria kali ambazo zinaweza kuwatia hatiani" alisema mwezeshaji na mwandishi Musa
Alisema kwa mujibu wa sheria mwandishi hapaswi kuandika habari za afya bila kuwa na chanzo sahihi na pia habari ya takwimu bila kuwa na mtaalamu anayehusika na masuala ya takwimu.
Mwenyekiti wa club ya waandishi wa habari, Zacharia Mtigani akimkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa waandishi hao ili waweze kuandika habari kwa usahihi.
Mgeni rasmi katika mafunzo hayo, Mkuu wa wilaya ya Babati, Lazaro Jacobo Twange, aliwataka waandishi wa habari kusoma sheria ili waweze kufanya kazi hizo kwa uadilifu.
Alisema tathnia ya habari ni muhimu kwa taifa lolote kwani ndio inayounganisha wananchi na Serikali yao jambo ambalo linarahisisha na kuleta mafanikio.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.